Mataifa 27 barani Afrika pia yaathiriwa na corona
Na AFP
BRAZAVILLE, Congo
NUSU ya nchi zote barani Afrika sasa zimeathiriwa na virusi vya corona, limesema Shirika la Afya Duniani (WHO).
Shirika hilo lilisema kuwa jumla ya nchi 27 zimeathiriwa kati ya mataifa 54 barani.
Afisi ya shirika hilo barani humu ilisema kuwa kufikia sasa, nchi hizo zimeripoti zaidi ya visa 300.
Shirika hilo lina makao yake jijini Brazaville, nchini Congo.
Kulingana na takwimu ilizotoa Jumanne, Misri ndiyo iliathiriwa zaidi ikiwa na visa 110, Afrika Kusini visa 62, Algeria visa 48 na Senegal visa 24.
Nchi zingine zilizoathiriwa ni Cameroon, Nigeria, Burkina Faso, Togo, DR Kongo, Cote d’Ivoire, Ghana, Gabon, Kenya, Ethiopia, Guinea, Rwanda, Namibia, Equatorial Guinea, Ushelisheli, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Congo, Mauritania , eSwatini, Liberia, Morocco, Tunisia na Sudan.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika barani humu, Dkt Matshidiso Moeti aliziomba nchi hizo kuchukua tahadhari za dharura, hasa baada ya virusi hivyo kutangazwa kuwa janga la dunia.
Aliziomba kuimarisha mikakati ya kukabiliana na maenezi yake.
“Huenda visa vya virusi hivi vikawa vichache barani Afrika. Hata hivyo, lazima serikali ziweke kila juhudi kuhakikisha kuwa zimedhibiti maambukizi yake,” akasema mkurugenzi huyo.
Na kuanzia Alhamisi, baadhi ya nchi zimetangaza kanuni kali, hasa kuhusu taratibu za usafiri.
Kwa mfano, Algeria imesimamisha usafiri wowote kuelekea Ulaya kuanzia kesho.
Afrika Kusini nayo imesema kuwa itafutilia mbali viza 10,000 ambazo zilikuwa zimetolewa kwa raia wa China na Iran katika miezi ya Januari na Februari.
Mataifa hayo ni miongoni mwa yale yaliyoathiriwa sana na virusi hivyo duniani.
“Tuko katika kiwango ambacho lazima tufanye kila juhudi kuhakikisha kuwa tumejilinda ifaavyo,” akasema Waziri wa Afya nchini humo Zweli Mkhize.
Taifa hilo limeripoti visa 62 ambapo vyote vinawajumuisha raia wa kigeni.
Maafisa wa afya wanachunguza visa ambapo watu wawili ambao ni raia wa nchi hiyo wanatuhumiwa kuambukizwa.
Nchini Somalia, taifa hilo lilipiga marufuku safari za ndege kutoka nchi za nje kuanzia jana, baada ya kuthibitisha kisa cha kwanza mnamo Jumanne.
Eneo kubwa la nchi hiyo bado linathibitiwa na kundi la al-Shabaab, ambalo limekuwa likiyashambulia makundi ya kutoa misaada kwa watu walioathiriwa na vita.
Wadadisi wanasema kuwa huenda ukosefu wa usalama ukaathiri juhudi za kukabili maenezi virusi nchini humo.