Matamshi ya Arati yalinikera, pikipiki yangu ilichomwa 2007, Osoro sasa ajitetea

Matamshi ya Arati yalinikera, pikipiki yangu ilichomwa 2007, Osoro sasa ajitetea

Na SAMMY WAWERU

Mbunge wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro amejitetea kuhusu kisa ambapo alipigana hadharani na mwenzake wa Dagoretti Kaskazini, Simba Arati.

Katika hafla ya mazishi ya babake naibu gavana wa Kisii Joash Maangi, Mzee Abel Gongera mnamo Jumatatu eneo la Kisii, wawili hao waliangushiana makonde.

Kulingana na Bw Osoro, matamshi ya Arati kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008 yalimghadhabisha.

Alisema akiwa mmoja wa waathiriwa wa ghasia na machafuko hayo, alihisi matamshi ya Arati yalifufua makovu ya aliyopitia kiasi cha kutostahimili.

“Arati alinichokoza, mimi ni mmoja wa walioathirika kufuatia ghasia hizo. Mojawapo ya pikipiki zangu niliyotumia kusukuma gurudumu la maisha Molo ilichomwa na wahuni, na nyingine kuibwa. Ni kutokana na machafuko hayo nilihama huko, nikaenda jijini Nairobi ambapo nilianza kuchuuza njugu,” Bw Osoro akasema.

Mazishi ya Mzee Gongera pia yalihudhuriwa na Naibu wa Rais William Ruto na kinara wa ODM Bw Raila Odinga.

Akizungumzia waombolezaji, Arati alisema viongozi na wanasiasa kutoka jamii ya Kisii wanaoegemea upande wa Dkt Ruto hawawakilishi msimamo wa jamii hiyo.

Mbunge huyo pia alionekana kumshambulia Naibu wa Rais, kwa kauli “jamii mbili pekee ndizo zimetawala Kenya tangu ipate uhuru, na ni wakati kuzipa mwanya jamii zingine pia kuwa uongozini”.

Dkt Ruto ameeleza bayana azma yake kuingia Ikulu 2022.

Ni kufuatia matamshi ya Arati, Bw Osoro alifika jukwaani na kumpokonya mikrofoni, wabunge hao wawili wakiishia kutwangana.

Maafisa wa polisi walilazimika kuingilia kati na kuwatawanya. Kitendo hicho cha aibu kinaendelea kukashifiwa.

Matamshi ya Bw Arati kuhusu jamii ambazo zimekuwa uongozini kuruhusu zingine kuwa mamlakani yanawiana na ya Rais Uhuru Kenyatta, aliyotoa Januari 2021 katika hafla ya mazishi ya mamake kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi, Mama Hannah Atsianzale.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali ikome kuhujumu vyama vya kutetea...

KINYUA BIN KING’ORI: Mabunge ya kaunti yasiwe na pupa...