Michezo

Matano aitaka Ingwe imfidie Sh4.9 milioni kwa kumsimamisha kazi

March 25th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Robert Matano anataka fidia ya Sh4.9 milioni kutoka kwa klabu ya AFC Leopards iliyomsimamisha kazi kabla ya kandarasi yake kumalizika.

Kulingana tovuti ya Goal, Matano, ambaye alijiunga na Ingwe tena mnamo Julai 10 mwaka 2017 baada ya kuinoa mwaka 2010 na 2011, ametumia kampuni ya mawakili ya Kiplagat & Company Advocates kushtaki waajiri hao wake wa zamani.

“Barua kutoka kwa kampuni hiyo, ambayo imeandikiwa maafisa wa Leopards, inaamrisha klabu hiyo ilipe Matano Sh700, 000 kwa kumfuta kazi, marupuru ya Sh63, 000 ya kushinda mechi ambayo hakuwa amelipwa na fidia ya kusimamishwa kazi kwa njia isiyofaa ya Sh350, 000 kila mwezi kwa miezi 12 (Sh4.2 milioni).

Ukijumlisha utapata Leopards inafaa kulipa Matano Sh4.9 milioni chini ya siku saba zijazo,” tovuti hiyo imenukuu mawakili hao wakisema.

Msimu huu, Matano aliongoza Leopards katika mechi tatu za ligi akipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Ulinzi Stars, sare ya 1-1 dhidi ya Posta Rangers na kulemewa 2-1 na Sofapaka.

Aliandikisha sare mbili katika mashindano ya Afrika ya Confederations Cup baada ya Ingwe kukabwa 1-1 mjini Machakos kabla ya kupiga sare tasa dhidi ya Fosa Juniors ya Madagascar.

Tangu Matano aondolewe majuma mawili yaliyopita, Leopards imepepeta SoNy Sugar 2-0, Mathare United 4-3, Wazito 3-2 na Kakamega Homeboyz 2-1 chini ya kocha Mtanzania Dennis Kitambi.