Michezo

Matano alia marefa walichangia timu yake kulimwa

August 15th, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Bandari FC Robert Matano amewalaumu vikali wasimamizi wa mechi ya KPL, Jumapili Agosti 12 waliyoipoteza 1-0  kwa wapinzani wao Bandari FC ugani Ruaraka mjini Nairobi.

Bao lake Yema Mwana katika kipindi cha kwanza lilitosha kuzamisha chombo cha mabingwa hao mara 11 wa KPL.

Bandari wameimarika sana tangu wamwaajiri Benard Mwalala kama mkufunzi wao na wemetwaa ushindi katika mechi tatu zilizopita dhidi ya timu ngumu kama Posta Rangers, Gor Mahia na Tusker FC.

Akichemkia mechi ya Jumapili, Matano alidai kwamba walionewa kwa kunyimwa mkwaju wa penalty na bao la wazi jambo lililochangia pakubwa kushindwa kwao.

“Usimamizi wa mechi ulikuwa mbovu sana na refa alichangia pakubwa kushindwa kwetu. Alitunyima penalti ya wazi na bao tulilolifunga kwa kudai kwamba mchezaji wetu aliotea. Kushindwa huku si mwisho wa dunia, tutapambana hadi mwisho kuhakikisha tumemaliza katika nafasi nzuri ligi ikifika tamati,” akawaka Matano.

Tusker msimu huu wanaonekana wamekula huu kwa kuwa wanashikilia nafasi ya 7 katika msimamo wa jedwali la ligi kwa alama 36 na tayari wamesalimu amri katika kutwaa ubingwa wa KPL walioushinda mara ya mwisho mwaka wa 2016.