Michezo

Matano kujitosa sokoni kusaka vipaji wa kuinyanyua Tusker

May 28th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Tusker FC, Robert Matano sasa anawazia kununua wachezaji wapya katika kidirisha cha uhamisho cha katikati ya ligi.

Udhaifu w Tusker umedhihirika katika mechi tatu zilizopita ambapo imetwangwa mfululuzi, kicho cha mwisho kikiwa 2-0 dhidi ya Kakamega Homeboyz wikendi katika uwanja wa Ruaraka, Nairobi.

Matano, ambaye alikuwa amelimwa na Kariobangi Sharks na Nakumatt kabla ya Jumamosi, aliachwa na machungu kwa kikosi chake baada ya matokeo hayo, akiapa kuwa atajitosa sokoni kusaka vipaji wa kufufua timu yake.

Kocha huyo alisema atafanya mageuzi kwa idara zote za usimamizi wa timu yake katika kipindi kifupi cha uhamisho. “Hatukufanya lolote leo lakini tunafaa kufanya jambo. Hatuwezi kuwa na wachezaji wazuri kama hawa na bado tunalemewa kushinda mechi.

“Lazima tupate wachezaji wazuri zaidi kwenye uhamisho. Sitabadilisha timu yote, lakini lazima tugeuza baadhi ya mambo. Tunahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuleta matokeo bora.

“Tunahitaji straika, ambaye anafuma mabao bila kuogopa madifenda, kiungo ambaye atatao mwongozo wa mechi na kipa mwenye uwezo wa kusimamisha mashuti makali,” akasema.