Michezo

Matano kumkosa difenda matata dhidi ya Kariobangi Sharks

May 9th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Tusker itakosa huduma za mlinzi wake matata Erick Ambunya katika mechi yao ya KPL siku ya Jumapili dhidi ya Kariobangi Sharks ugani Ruaraka.

Difenda huyo ambaye anatumikia marufuku ya mechi moja amekuwa mhimili mkubwa kwa wanamvinyo hawa walioonyesha ufufuo mkubwa tangu kocha Robert Matano apokezwe mikoba ya kuiongoza.

Ambunywa alilishwa kadi nyekundu katika mtanange wa ligi Jumapili iliyopita dhidi ya Klabu ya Bandari mechi iliyogaragazwa ugani Mbaraki. Tusker walishinda mechi hiyo kwa mabao 2-0.

Tangu ujio wa Kocha Matano, klabu hiyo imerekodi asilimia 100 ya ushindi kati mechi zake tatu. Iliwalambisha klabu ya SoNy Sugar mabao 3-2 , ikawachabanga Wazito FC 1-0 na ushindi waliousajili Jumapili iliyopita dhidi ya Bandari FC ulizidi kudhihirisha ubabe wao.

Kocha huyo kwa jina la utani ‘the lion’ alichukua usimamizi wa Tusker FC kutoka kwa aliyekuwa kocha raia ya  Uganda Sam Timbe.

Msimu huu klabu hiyo ilikuwa ikipata matokeo mabaya chini ya kocha Timbe na wakati mmoja ilikuwa ikiselelea katika eneo hatari la kuteremshwa ngazi kwenye msimamo wa jedwali la ligi.

Ushindi  huo katika mechi tatu mfululizo umewapaisha mabingwa hao wa zamani hadi nafasi ya tisa kwa alama 19 nane tu nyuma ya viongozi wa ligi Gor Mahia.

Wapinzani wao katika mechi ya Jumapili Kariobangi Sharks wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama 17 na imesajili matokeo ya wastani ya sare katika mechi zake tatu zilizopita.