Habari MsetoSiasa

Matapeli wa dhahabu feki washtakiwe Uarabuni – Gavana Mutua

May 22nd, 2019 2 min read

PIUS MAUNDU na RUTH MBULA

GAVANA wa Machakos Dkt Alfred Mutua Jumatano alipendekeza kwamba washukiwa kwenye sakata ya dhahabu bandia washtakiwe Uarabuni badala ya hapa nchini.

Sakata hiyo inajumuisha kampuni inayohusishwa na mwanamfalme wa Uarabuni inayodaiwa ilihadaiwa zaidi ya Sh1bilioni na walaghai kutoka Kenya waliojifanya wana uwezo wa kuwauzia dhahabu kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kulingana na Dkt Mutua, haki itapatikana tu iwapo washukiwa watashtakiwa katika korti za Dubai na wakipatikana na hatia waachwe wasote kwenye magereza ya huko.

Hata hivyo, Dkt Mutua alimtetea Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ambaye amehusishwa na sakata hiyo akisema analengwa kisiasa.

Kinara huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap pia alipendekeza washukiwa wa sakata hiyo wafanyiwe uchunguzi wa mtindo wa maisha ili utajiri walioupata kwa njia ya ufisadi utwaliwe na serikali kabla hawajasafirishwa Dubai kukabili mashtaka.

Dkt Mutua alitoa kauli hiyo jana kupitia taarifa aliyotuma kwa vyombo habari na akataka sakata hiyo ambayo imekuwa ikiangaziwa sana kwenye vyombo vya habari isisababishe vita vilivyokuwa vikiendelea dhidi ya ufisadi vipoteze dira.

“Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na asasi nyingine za uchunguzi hazifai kupoteza mwelekeo kwenye vita dhidi ya ufisadi na kuwacha kuangazia sakata kubwa zilizogubika taifa siku za nyuma. Hata tukiangazia sakata ya dhahabu, asasi husika hazifai kusahau sakata za awali,” ikasema taarifa ya Dkt Mutua.

Uchunguzi kuhusu malipo yanayotiliwa shaka kwenye miradi ya mabwawa ya Arror na Kimwarer, na ufisadi kwenye Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) ni kati ya sakata kubwa zilizokuwa zikiendelea kabla ya kuchipuka kwa sakata ya dhahabu bandia.

Wakati uo huo, Gavana wa Nyamira John Nyangarama amewakashifu wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kumtaka Dkt Matiang’i ajiuzulu kuhusiana na sakata ya dhahabu.

Bw Nyangarama alisema kundi la Tangatanga halifai kuruhusiwa kuendelea kutoa matamshi yanayozidisha joto la kisiasa nchini huku akiwataka kutoa ushahidi unaothibitisha kwamba Dkt Matiang’i alihusika na sakata hiyo.

“Nawaomba viongozi watathmini semi zao na kuwa tayari kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuibuka na madai mazito ili wasichukuliwe kama wanaolifanyia madai hayo mzaha,” akasema Gavana huyo wa chama cha ODM.

“Hawa wanasiasa wa kundi la Tangatanga wanatoa matamshi yasiyofaa dhidi ya watu wanaodai ni wapinzani wao. Hiyo njia wanayoifuata imetumbukiza taifa hili kwenye machafuko jinsi tulivyoona katika siku za nyuma.

“Sisi tunakubaliana nao kwamba watakaopatikana na hatia wanafaa kuhukumiwa ila hatutakubali madai ya kiholela bila ushahidi. Wadhibiti ndimi zao na kuchunguza mambo kabla ya kutoa semi zao hadharani,” akaonya Bw Nyangarama.