Habari Mseto

Matarajio ya wafanyabiashara bajeti ikisomwa

June 11th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

USHURU wa bidhaa mbalimbali upunguzwe zaidi ili kuzipa biashara afueni wakati huu janga la Covid-19 linaendelea kuziyumbisha.

Hili ndilo ombi la wafanyabiashara, huku Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa Ukur Yattani Alhamisi akisoma makadiro ya bajeti mwaka wa fedha 2020/2021.

Macho yote yakielekezwa katika bunge la kitaifa, anakosomea Waziri makadirio hayo ya matumizi ya fedha kipindi cha mwaka mmoja ujao, wafanyabiashara wanalia biashara zao kuathirika kwa kiasi kikuu, hasa tangu Kenya itangaze kisa cha kwanza cha Covid-19 Machi 13, 2020.

Baadhi ya wafanyabiashara tuliozungumza nao, wanaiomba serikali kupunguza zaidi ushuru (VAT) wa bidhaa, ili kuwapa afueni.

“Biashara zimeathirika, uchumi umezorota, tangu virusi vya corona vitue nchini. Tunahimiza serikali serikali ipunguze VAT zaidi ili kutunusuru,” Antony Wanjiru, mfanyabiashara Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi, ameambia Taifa Leo katika mahojiano.

Mfanyabiashara Antony Wanjiru. Picha/ Sammy Waweru

Mei 2020 Rais Uhuru Kenyatta alitoa kiasi cha Sh53.7 bilioni kupiga jeki uchumi, kufuatia athari za janga la corona.

Rais pia alitangaza kupunguza VAT kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14.

Licha ya afueni hiyo ya muda, Bw Antony ambaye ni mmiliki wa duka la bidhaa mbalimbali, zikiwemo za kula, na pia huduma za M-Pesa, anasema hajahisi kuondolewa mlima wa mzigo unaosababishwa na hali ngumu ya maisha inayochangiwa na virusi vya corona.

“Tuliskia kwenye vyombo vya habari vya kielektroniki na kusoma magazetini kwamba kuna fedha zilizotolewa kunusuru uchumi, ila hatuoni mabadiliko yoyote. Mambo yanazidi kuwa magumu,” akasema mfanyabiashara huyo.

Kauli yake inawiana na ya Annitah Wairimu, muuzaji wa nguo, anayesema gharama ya biashara imepanda kwa kile anataja kama nguo kuwa ghali kutokana na uhaba unaosababishwa na Covid-19, ugonjwa ambao sasa ni janga la kimataifa.

“Biashara zinafilisika kwa sababu ya athari za corona. Tunaomba serikali angalau itathmini ushuru,” Wairimu akasema.

Virusi vya corona na ambavyo kwa mara ya kwanza viliripotiwa Mjini Wuhan, China, vimeathiri uchumi na sekta mbalimbali, katika kila dira ya ulimwengu. Kwa kauli moja, Wakenya wanaomba bajeti itayosomwa iwaletee afueni.

Waziri Yatani anasoma makadirio ya bajeti ya Sh2.790 trilioni, mwaka wa Fedha 2020/2021.

Inasomwa wakati ambapo Kenya imekodolewa macho na janga hatari la Covid – 19, mafuriko na nzige. Kiasi kikubwa cha bajeti hiyo kinapaniwa kuelekezwa kudhibiti janga la corona.

Kufikia sasa Kenya ina deni la mikopo zaidi ya Sh6 trilioni, ikizingatiwa kuwa bunge la kitaifa mwaka uliopita liliongeza kiwango cha fedha zinazoweza kukopwa kuwa Sh9 trilioni.

Bw Yatani jana Jumatano kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini, alinukuliwa akieleza: “Hakuna taifa linaloweza kuendesha miradi ya maendeleo bila mikopo.”