Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Matatizo yanayowakumba walimu kutokana na matumizi ya lugha ya kigeni katika kufundishia shuleni

April 5th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

TUNAANGAZIA changamoto zinazowakabili walimu kutokana na hali ya kukosa kutumia Kiswahili katika ufundishaji wa elimu ya sekondari.

Tatizo mojawapo linalojitokeza ni kutofuata sera ya elimu kuhusu lugha ya kufundishia elimu ya sekondari.

Wanaisimu Gorham na Ruberg (1985) wanadai kwamba sera ya lugha ya kufundishia nchini Angola inakipe Kireno kipaumbele ingawa walimu huchanganya na lugha za wenyeji wanapofundisha madarasani.

Hali hii ni changamoto kubwa kwa walimu nchini humo kwa sababu itakuwa vigumu kufafanua dhana kamili ya somo kama inavyotakiwa.

Yamkini sera ya elimu nchini Angola haifuatwi kikamilifu.

Katika Afrika ya Kati hali inafanana na ilivyo nchini Angola. Kwa mujibu wa McIntyre (1985) sera ya elimu nchini humo inatamka kuwa lugha ya kufundishia ni Kifaransa. McIntyre anafafanua kuwa walimu nchini humo hukumbwa na changamoto za mawasilino darasani.

Walimu hutumia Kifaransa na Kisango ambayo ni lugha ya wenyeji. Kutokana na hali hiyo, sera ya elimu haifuatwi na badala yake inavurugwa.

Mekacha (2000) anabaini kwamba idadi kubwa ya wanaotoa mafunzo ya ngazi ya sekondari nchini Tanzania hawana weledi wa lugha ya Kiingereza unaotakiwa kulingana na mahitaji ya viwango vyao, hivyo hulazimika kuchanganya lugha mbili darasani.

Hali hii inachangia kushusha kiwango cha elimu nchini Tanzania na ni changamoto kubwa kwa walimu kwa sababu itakuwa vigumu kwa mwalimu kumaliza mada zilizo kwa muhtasari ikiwa atatumia lugha mbili.

Ni bayana kwamba pana umuhimu wa suala hili kufanyiwa utafiti wa kina ili kubuni mbinu za kusuluhisha changamoto hizo na kutekeleza sera ya elimu kikamilifu. Watafiti mbalimbali wamebuni nadharia anuai katika tafiti zao kuhusu lugha ya kufundishia.

 

Ili kuwasiliana na mtaalamu, mwandikie kwa baruapepe: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education.In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5. New York: Springer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.