Habari

MATATU: Matiang'i na Boinnet waapa kutolegeza kamba

November 13th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

SERIKALI Jumatatu iliapa kutolegeza kamba hadi magari yote ya umma yazingatie sheria za barabarani maarufu kama Sheria za Michuki huku shughuli za usafiri zikilemazwa baaada ya wenye magari kuyaondoa magari yao barabarani wakilalamikia kutekelezwa kwa sheria hizo.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiangi, mwenzake wa Uchukuzi James Macharia na Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet waliungana kusisitiza kwamba ni magari yatakayotimiza sheria hizo tu ndiyo yatakayoruhusiwa kurejea barabarani huku wakikemea hatua ya kuongezwa marudufu kwa nauli na wahudumu wa magari machache yaliyokuwa barabarani.

“Nimesikia kuwa baadhi ya wenye magari wameondoa magari yao barabarani. Wanaweza kukaa nayo wanavyotaka kwa sababu nasi hatutalegeza kamba,” akasema Dkt Matiang’i.

Akizungumza wakati wa kushuhudia ukaguzi wa magari katika kituo cha ukaguzi cha Likoni jijini Nairobi, Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet alithibitisha kwamba madereva na utingo 2,000 jana walikamatwa kwa kutotii sheria hizo na watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka mbalimabali.

“Hatutalegeza kamba hadi magari yote yathibitishwe kuwa salama kuwahudumia abiria kupitia ukaguzi huu na kwa kuweka vifaa vinavyofaa. Tayari tumewanasa wahudumu 2000 na watakabiliwa vikali kisheria wala hatutokoma hadi tufikie malengo yetu,” akasema Bw Boinnet.

Awali katika kituo cha reli cha Railways, Waziri wa Uchukuzi James Macharia aliwaongoza maafisa wa shirika la reli nchini kukagua kituo hicho na akaamrisha idadi ya treni zinazohudumu jijini Nairobi ziongezwe kutoka 12 hadi 18 kila siku ili kukidhi idadi kubwa ya wasafiri wanaolazimika kupiga guu au kugharamika zaidi hadi maeneo yao ya kazi kutokana na ukosefu wa magari.

Vilevile Bw Macharia aliamrisha Mamlaka ya kitaifa ya uchukuzi nchini (NTSA) ifutilie mbali leseni za vyama vya ushirika vya wamiliki magari ya umma walioyaondoa magari yao barabarani kama njia ya kupinga kutekelezwa kwa Sheria za Michuki.

“Mara hii lazima vita hivi vifaulu liwalo na liwe ili tusishuhudie ajali nyingi msimu wa Krismasi jinsi ilivyokuwa mwaka jana. Lengo letu ni kuyaokoa maisha ndiposa tunawarai wananchi wakumbatie usafiri wa garimoshi ambao ni nafuu na nauli yake itapunguzwa kwa asilimia 10 kipindi hiki, sekta ya usafiri inapokumbwa na matatizo,” akasema Dkt Macharia.

Kauli za viongozi hao wa serikali zilijiri wakati wananchi kutoka mitaa mbalimbali wakilazimika kutembea kwa miguu au kulipa nauli mara tatu zaidi baada ya wenye magari kugoma.

Umati mkubwa wa wasafiri ulionekana ukitembea katika barabara za Jogoo, Mombasa, Thika Super Highway, Westlands, Lang’ata na Ngong huku waliobahatika kupata magari wakilazimika kulipa nauli mara mbili au tatu zaidi.

“Nimelipa Sh450 kutoka Ngong na kawaida sisi hulipa Sh150 au ikienda sana Sh200. Hata hivyo, naunga mkono serikali katika vita hivi ili tatizo hili litatuliwe mara moja na barabara zetu ziwe salama,” akasema abiria mmoja.