Habari za Kitaifa

Matatu ya abiria 14 yanaswa ikibeba wanafunzi 31!

March 30th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MAAFISA wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) katika Kaunti ya Meru wamenasa matatu moja ya viti 14 vya abiria ikibeba wanafunzi 31.

Kulingana na taarifa katika ukarasa wake wa mtandao wa X, mamlaka hiyo inasema wanafunzi hao walikuwa wametoka shule moja katika kaunti.

NTSA ilisema dereva wa gari hilo alitoroka na juhudi za kumsaka zinaendelea.

Matatu hiyo imepelekwa katika kituo kimoja cha polisi mjini Meru huku wanafunzi hao wakitafutiwa usafiri mbadala.

Kuanzia mwanzani mwa wiki hii inayokamilika, maafisa wa NTSA walianzisha msako mkali dhidi ya magari yanayokiuka sheria za trafiki katika barabara kadhaa humu nchini.

Hii ni kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen kama njia ya kukomesha ongezeko la ajali za barabarani.

Visa hivyo, vimeongezeka nchini tangu Januari 2024 na kufikia sasa, watu 1,067 wameangamia katika ajali za barabarani miongoni mwao wakiwa wanafunzi wa shule na vyuo vya elimu ya juu.

Mnamo Ijumaa, NTSA ilisitisha matumizi ya leseni za kazi za mashirika mawili ya huduma za matatu (Saccos) kwa kukiuka sheria za barabarani.

“Saccos hizo zilifeli kuzingatia hitaji la Sehemu ya 5 ya kanuni za NTSA kuhusu huduma za magari ya uchukuzi wa abiria ya 2014. Aidha, magari ya Saccos hizo yalikiuka kanuni kuhusu mwendo kasi unaokubalika na NTSA,” NTSA ikasema.