Habari Mseto

MATESO: Atwoli ataka ajira za Uarabuni zichunguzwe

January 28th, 2019 1 min read

Na Winnie Atieno

MUUNGANO wa wafanyakazi nchini (Cotu) unamtaka Rais Uhuru Kenyatta kufuatilia ajira za wafanyakazi wa nyumbani katika nchi za Uarabuni.

Katibu Mkuu wa muungano huo, Bw Francis Atwoli alisema jana kuwa Wakenya wanaendelea kuteseka Uarabuni wanapoenda kusaka kazi.

“Wanafanywa watumwa, ni madhila ambayo hata kama ni umaskini haina haja kumpeleka mtoto wako Uarabuni kuteseka. Wengine wanarudi wakiwa kwenye jeneza,,” akasema Bw Atwoli.

Alimtaka Rais kuingilia kati suala hilo baada ya wizara ya Leba kutia mkataba na Saudi Arabia kuhakikisha wafanyakazi wa humu nchini wanapewa mazingira bora ya kufanya kazi. Lakini akiongea huko Mombasa, katika hoteli ya Whitesands, Bw Atwoli aliitaka serikali kuweka mikakati ya kufungua ajira humu nchini badala ya Wakenya kwenda kufanya kazi uarabuni.

Mwaka wa 2014 serikali ilipiga marufuku ajira nchini humo na kufunguliwa upya mwaka 2017, huku serikali ikisisitiza umuhimu wa ukaguzi wa ajenti za ajira.

“Kuruhusu nchi hiyo kuwasajili wakenya kufanya kaiz huko Uarabuni kutaongeza madhila ya watoto wetu. Nina wasiwasi kuwa waziri wa Leba amekubali na hata kutia saini,” akasema.

Pia aliwashtumu maajenti wanaowasajili wakenya kufanya kazi uarabuni bila ya kujali maslahi yao wanapokumbwa na matatizo.