Mateso ya polisi aliyepata upofu akiwa kazini

Mateso ya polisi aliyepata upofu akiwa kazini

NA FARHIYA HUSSEIN

AFISA wa polisi wa zamani aliyepoteza uwezo wa kuona baada ya shambulio kutokea katika kituo alipokuwa akifanya kazi, amelalamikia hali ngumu ya maisha inayomkumba na familia yake.

Bw Alex Charo, alikuwa akifurahia manufaa ya kuajiriwa kama afisa wa kiserikali hadi jioni ya Agosti 28, 1998 wakati mashambulizi yalipotokea katika kituo cha polisi cha Marereni, Kaunti ya Kilifi.

Katika shambulio hilo la kihalifu, alipata majeraha mabaya ambayo yalimsababishia upofu wa macho yote mawili.

Kulingana na Bw Charo, alihitimu kutoka Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo na kupata kazi katika kikosi cha polisi cha Lang’ata mwaka wa 1987.

Baadaye, alihudumu katika vituo vya polisi vya Karen (Nairobi), Nyali (Mombasa) na Malindi (Kilifi) mtawalia.

“Baada ya hapo, nilifanya katika kituo cha polisi cha Marereni kilichoko Kilifi mwaka wa 1998,” akaeleza Bw Charo.
Siku ya shambulio hilo, alikuwa afisa wa zamu katika kituo cha polisi.

“Ilikuwa mwendo wa saa moja usiku washambuliaji walipovamia kituo cha polisi. Waliingia kupitia kwa madirisha. Walikuwa takriban 15 wakiwa wamejihami na silaha,” akasema Bw Charo, akieleza kuwa alipata jeraha la kichwa baada ya kupigwa risasi.

Jeraha hilo ndilo liliathiri macho yake yote mawili.

“Nilijaribu kila nilichoweza, na nilitembelea hospitali tofauti ili kutafuta matibabu ya kurejesha uwezo wa kuona lakini sikufanikiwa. Niliwaandikia wakubwa wangu barua kadhaa kuomba msaada wa matibabu lakini walinishauri nijiandikishe katika shule ya vipofu,” alisema Bw Charo.

Kwa kufuata ushauri huo, alijiunga na shule ya vipofu iliyo Kaunti ya Machakos.

Kwa miaka miwili chuoni humo, alijifunza kozi ya kusoma, kuandika na ujuzi wa kijamii na kujitegemea, masomo ya vipofu na kisha kuhitimu baada ya kupata alama ya A.

Bi Constance Chivatsi, mkewe, anakumbuka taabu walizopitia baada ya mumewe kupoteza uwezo wa kuona.

“Siku ambayo alishambuliwa nilikuwa na ujauzito wa miezi sita wa mtoto wetu wa pili. Ilibidi niingilie kati na kutafutia familia yetu riziki. Nilifanya kazi kwenye maeneo ya ujenzi na kuchukua kazi nyingine za mikono ili kuhakikisha watoto hawakosi shule. Maisha ikawa ngumu, nakumbuka wakati mmoja mume wangu alijaribu kujitoa uhai. Mambo yamekuwa magumu kwetu,” akasema Bi Chivatsi.

Bw Charo ambaye amestaafu na anategemea malipo ya uzeeni amewataka Rais William Ruto na Inspekta Jenerali wa Polisi kuangazia kesi yake, akisema alikuwa na sifa nzuri alipokuwa kazini.

Katika barua yake kwa kamishna wa polisi, Bw Charo anaomba kulipwa kimaalumu kwa sababu za matibabu akiwa ametumikia kikosi cha polisi kwa miaka 18.

“Ninalipwa kama mstaafu chini ya kustaafu mapema lakini kiwango cha jeraha langu kilielezewa na bodi ya matibabu kama asilimia 100 ya jeraha la jicho ambalo ni upofu wa kudumu. Naomba ofisi yako ilichukulie suala hilo kama la dharura kwa kuwa mimi ni kipofu na nina wategemezi sita wa kulisha na kuelimisha,” ilisoma barua hiyo.

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Alitalii, akapata wazo la kuuza utalii na...

NJENJE: Hasla Fund yanyofolewa Sh40 bilioni kinyume na...

T L