Michezo

Mathare na Ulinzi waimarika katika mapambano KPL

February 26th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU za Mathare United, SoNy Sugar na Ulinzi Stars pamoja na Mount Kenya United ndizo timu zilizoimarika kwenye Ligi Kuu inayoongozwa na Bandari baada ya mechi za raundi ya 15 kusakatwa wikendi iliyopita.

Washindi wa mwaka wa 2008 Mathare, ambao walikuwa wamepoteza mwelekeo katika mechi tano, walirejelea kushinda na kuimarisha alama zao hadi 29 baada ya kuchabanga mabingwa mara 13 AFC Leopards 2-0 mjini Machakos.

James Kinyanjui wa Mathare United (kushoto) apambana kuupata mpira kutoka kwa mvamizi Whyvonne Izuza wa AFC Leopards katika mchuano wa Ligi Kuu ya KPL iliyowakutanisha ugani Kenyatta, Machakos. Picha/ Sila Kiplagat

Ushindi huu uliinua Mathare juu ya mabingwa watetezi Gor Mahia ambao hawakuwa na mechi ya ligi wikendi. Mathare ya kocha Francis Kimanzi iko alama mbili nyuma ya Bandari, ambayo ilizoa ushindi wake wa tatu mfululizo ilipocharaza Nzoia Sugar 1-0 katika mechi yake ya 14 mjini Mombasa.

Mabingwa mara 17 Gor wameteremka hadi nafasi ya tatu. Vijana wa Hassan Oktay wana alama 26 kutokana na mechi 13. Wataalika mabingwa mara 11 Tusker hapo Jumatano.

Tusker hawakuwa na mechi wikendi. Wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 25. Mechi dhidi ya Gor ni yao ya 14. Mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka wanafunga tano-bora kwa alama 24 baada ya kutoka 2-2 dhidi ya Kakamega Homeboyz uwanjani Bukhungu.

Washindi wa Kombe la Ngao Kariobangi Sharks hawajasonga kutoka nafasi ya sita baada ya kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Vihiga United uwanjani Bukhungu.

Sharks wana alama 22 sawa na nambari saba SoNy, ambao wamesakata mechi moja zaidi. Wanasukari wa SoNy walishinda mchuano wao wa raundi ya 15 kwa kupepeta Western Stima 4-0 mjini Awendo. Ushindi huo wao wa pili mfululizo uliwawezesha kubadilishana nafasi na Stima, ambao wameshuka hadi nafasi ya nane wakiwa wamejizolea alama 21 kutokana na mechi 14.

Wanaumeme wa Stima walikuwa wamekaba Gor 1-1 Jumatano.

Stima wanafuatiwa na Homeboyz waliokusanya alama 18 kutokana na mechi 15.

Wanajeshi wa Ulinzi wamezidiwa na Homeboyz kwa tofauti ya magoli katika nafasi ya 10. Walikubali sare ya 1-1 dhidi ya Posta Rangers.

Ulinzi walirukia nafasi ya 11 na kusukuma Nzoia nafasi moja chini katika nafasi ya 12 kwa alama 17, ingawa wanasukari hawa wamecheza mechi moja chache. Nzoia iko alama moja mbele ya nambari 12 KCB iliosakata mechi 15.

Alama moja

Alama moja inatofautisha KCB na nambari 13 Rangers, ambayo imejizolea 15. Nambari 14 ni Chemelil iliyotoka sare ya 1-1 dhidi ya KCB.

Ina alama 14 kutokana na mechi 14. Zoo imekwamilia nafasi ya 15 kwa alama 12. Mount Kenya United ilirukia nafasi ya 16 kutoka mkiani baada ya kulima Zoo 1-0.

Vihiga na Leopards zimeteremka chini nafasi moja kila mmoja. Zinashikilia nafasi za 17 na 18 kwa alama 11 na 10 baada ya kusakata mechi 15 na 14, mtawalia.

Vihiga haina ushindi katika mechi 14 nayo Leopards imepoteza michuano sita mfululizo.