Michezo

Mathare United, Tusker zasajili ushindi

March 8th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Mathare United, Western Stima, Tusker na Bandari walikuwa na siku nzuri Jumamosi uwanjani baada ya kuzoa ushindi kila mmoja kwenye Ligi Kuu.

Uwanjani Kasarani, mabingwa wa mwaka 2008 Mathare, ambao hawakuwa na ushindi katika mechi mbili zilizopita, wamelipua Kisumu All Stars 4-1 kupitia mabao ya Kevin Kimani, Clifford Alwanga, Daniel Otieno na Tyson Otieno.

Wageni Kisumu walipata bao lao kupitia kwa Eric Otieno.

Stima, ambayo ilikuwa imekamilisha mechi saba bila ushindi, ilitumia uwanja wake wa nyumbani wa Moi mjini Kisumu kwa kuzamisha Posta Rangers 2-0.

Uwanjani Ruaraka, wenyeji Tusker walizima Chemelil Sugar 2-0 kupitia mabao ya Timothy Otieno, ambaye sasa amepiku John Makwata kwa bao moja.

Imechukua zaidi ya mwezi mmoja kwa Makwata kupitwa katika ufungaji wa mabao tangu ahamie Zesco United nchini Zambia kutoka AFC Leopards mnamo Januari 31.

Naye John Mwita aliendelea kuonyesha uweledi wake wa kuchana nyavu alipofungia Bandari bao la pekee ikizidia nguvu Kariobangi Sharks 1-0 uwanjani Mbaraki mjini Mombasa.

Mwita sasa amefunga mabao matatu katika mechi mbili baada ya kutikisa nyavu mara mbili Bandari ikikanyaga KCB katika mechi iliyopita.

Mechi katika ya Nzoia Sugar na KCB imetamatika 0-0 uwanjani Sudi mjini Bungoma, sawa na ile iliyokutanisha Wazito na Ulinzi Stars uwanjani Kenyatta mjini Machakos.