Makala

MATHEKA: Ajabu Kenya kubezwa na majirani licha ya ukarimu

December 16th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA miaka mingi Kenya imekuwa karimu kwa kukaribisha raia wa nchi jirani zake wanaotoroka ghasia za kikabila na kisiasa katika nchi zao.

Hata hivyo, nchi hizi zimekuwa zikilipa ukarimu huu kwa dhuluma nitakavyoeleza kwenye makala haya.

Kwanza, ukarimu wa Kenya umeifanya kuwa na kambi mbili kubwa za wakimbizi Daadab Kaunti ya Garissa na Kakuma Kaunti ya Turkana. Kambi ya Dadaab ina wakimbizi wengi kutoka Somalia na Ethiopia na Kakuma ina wakimbizi kutoka Ethiopia, Sudan Kusini, Burudi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Rwanda.

Mbali na kupokea wakimbizi, utulivu nchini huwa unavuta raia kutoka nchi jirani kuishi na kufanya kazi na biashara. Ukarimu wa Kenya umeifanya kuchangia katika juhudi za kurejesha amani katika nchi zinazokumbwa na ghasia kama Somalia ambako ilituma wanajeshi kuangamiza magaidi wa Al-Shabaab ambao kwa miaka mingi walikuwa wamehangaisha nchi hiyo na kuthibiti kila sekta.

Nchi hiyo haikuwa na serikali hadi wanajeshi wa Kenya walipoungana na wa Muungano wa Afrika kusaidia kubuni iliyopo kwa sasa na iliyotangulia.

Wanaofuatilia historia ya Afrika Mashariki kwa makini watabaini kwamba Kenya ilitekeleza jukumu muhimu kurejesha amani nchini Uganda miaka ya sabini na themanini.

Raia wa nchi hiyo walivuka mpaka na kukimbilia Kenya hasa wakati wa utawala wa dikteta Idi Amin Dada aliyekuwa akiwasaka na kuwaua wapinzani wake.

Hali ilikuwa hivyo wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan wakati raia wa Sudan Kusini walipotorokea Kenya wakihofia usalama wao.

Hata baada ya Sudan Kusini kupata uhuru kutoka kwa Sudan, Kenya imekuwa msitari wa mbele kupatanisha pande zinazopigana. Hata hivyo, ukarimu huu umekuwa ghali mno kwa Kenya huku nchi inazosaidia zikigeuka na kudhulumu raia wake, kuzua ugomvi wa kidiplomasia usio na maana.

Badala ya kuheshimu Kenya kwa kutumia rasilmali zake kusaidia raia wake, mataifa hayo na raia wake wamekuwa wakidharau nchi yetu waziwazi.

Kwa mfano, Somalia ilishtaki Kenya katika Mahakama ya kimataifa kuhusu Haki (ICJ) kuhusu mzozo wa eneo lenye utajiri wa gesi katika bahari Hindi. Juzi ilizua mzozo mpya kwa kutimua balozi wa Kenya nchini humo.

Japo mizozo huzuka kati ya nchi, kwa kuzingatia msaada ambao Kenya imepatia nchi hiyo, ikiwa sehemu ya jamii ya kimataifa na kama jirani, mzozo huo ungetatuliwa kupitia mazungumzo kati ya nchi hizi mbili.

Licha ya Uganda kutegemea Kenya kwa huduma muhimu ikiwemo kusafirisha bidhaa kutoka au kuingiza nchi hiyo, ilivamia kisiwa cha Migingo kwenye ziwa Victoria na imekuwa ikihangaisha wavuvi kutoka Kenya katika ziwa hilo.

Sio mara moja wavuvi wa Kenya wamekamatwa na maafisa wa usalama wa Uganda na kuachiliwa baada ya kutozwa faini kubwa.

Aidha, kumekuwa na mzozo kati ya mpaka wa Kenya na Tanzania, wafugaji wakipokonywa mifugo wao na maafisa wa usalama wa Tanzania.

Chambilecho wahenga, asante ya punda ni mateke.