MATHEKA: BBI inafaidi wanasiasa pekee mzigo ukiwa kwa raia

MATHEKA: BBI inafaidi wanasiasa pekee mzigo ukiwa kwa raia

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga za kubadilisha katiba kupitia mpango wao wa maridhiano (BBI) zinaelekea kufaulu baada ya mabunge ya kaunti zaidi ya 40 kuidhinisha mswada wao.

Jinsi mabunge zaidi ya 20 yalivyopitisha mswada huo kwa mpigo Jumanne katika vikao vilivyohudhuriwa au kuungwa na magavana wa kaunti inaonyesha kuwa vinara wa mchakato huo na washirika wao waliwasukuma wahakikishe haukufeli.

Hii ni baada ya kuwashawishi madiwani kwa ruzuku ya Sh2 milioni kununua magari kama chambo ili waweze kuunga mswada huo.

Baada ya kupitishwa na mabunge ya kaunti, vinara hao wanatarajia kwamba awamu zilizobaki zitakuwa mteremko. Kile ambacho Wakenya wanafaa kufahamu, ni kwamba japo watetezi wa mswada huo wanasema unalenga kuunganisha Wakenya, ukweli ni kwamba unalenga kuunganisha viongozi wa kisiasa na washirika wao ambao wanawania nyadhifa zitakazobuniwa za waziri mkuu, manaibu waziri mkuu, kiongozi wa upinzani na ubunge kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wabunge.

Wanasiasa hao pia wanaunga mchakato huo wakilenga kuteuliwa mawaziri, mabalozi na katika nyadhifa nyingine za uongozi serikalini.

Mapendekezo ambayo raia wanaambiwa kwamba yanalenga kuwanufaisha kama vile kuongeza mgao kwa serikali za kaunti, kupatia vijana afueni ya kulipa kodi wakianzisha biashara na ya masomo ya hali ya juu, ni hekaya za abunuwasi.

Hivi ni vishawishi ambavyo, mswada huo ukipita kwenye kura ya maamuzi, vitasahaulika. Kilicho wazi na ambacho Wakenya wanaounga na wasiounga hawataepuka ni kubeba mzigo zaidi baada ya katiba kubadilishwa.

Mzigo huo utakuwa ni kulipa kodi zaidi kulipa mishahara na kufadhili ofisi mpya zitakazobuniwa. Hawa ndio Wakenya ambao wanaahidiwa afueni ya kutolipa ushuru wakianzisha biashara ilhali serikali itahitaji pesa za kuendesha ofisi ya waziri mkuu, manaibu wake wawili, kiongozi wa upinzani rasmi na wabunge zaidi ya 100.

Kwa kuzingatia mazingira ya siasa nchini kwa wakati huu, ni wazi kuwa mabadiliko ya katiba yanayopendekezwa yatapitishwa kwenye kura ya maamuzi kwa vyovyote vile, sio kwa sababu inawafaidi Wakenya wanavyoahidiwa, bali ni kuwa wanaambiwa inawafaidi ilhali ilikuwa wazo la watu wawili pekee walio na ushawishi.

Katika mazingira ambayo mabadiliko hayo yanafanyika, hasa miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu, kuna kila dalili kwamba hayanuiwi kunufaisha mwananchi wa kawaida mbali mwananchi wa kawaida anatumiwa kuyaidhinisha tu yatimize maslahi ya wanasiasa wachache.

You can share this post!

Faki ataka nakala za BBI kwa Kiswahili

OMAUYA: Kauli ya Ruto: ‘nichukie ila swara tutamla hadi...