Makala

MATHEKA: BBI si ya kusaidia raia, ni ya kufaa wanasiasa

October 23rd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

NIMEKUWA nikifuatilia kwa makini mjadala kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano maarufu kama BBI ambalo wanalolipigia debe wanasema linalenga kuunganisha Wakenya.

Kulingana nao, mapendekezo ya jopo hilo yakitekelezwa, Wakenya hawatakuwa wakipigana wakati wa uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

Wanasema kuwa hili linaweza kuafikiwa kupitia mfumo wa serikali wa ubunge ikiwa na Waziri Mkuu na pengine manaibu wawili na mawaziri kuwa wabunge.

Kuna wanaohisi kuwa mfumo wa ugatuzi unafaa kurekebishwa kuwe na majimbo 14 au manane badala ya 47.

Kwa maoni yangu, ikiwa haya ndiyo mapendekezo yanayodaiwa kuwa ya kuunganisha Wakenya, basi nchi hii itakuwa imechukua mwelekeo hatari.

Kwanza, kwa kupunguza idadi ya majimbo kutoka 47 hadi 14, itakuwa ni kurudisha nyuma hatua ambazo nchi imepiga miaka saba baada ya kukumbatia ugatuzi.

Mfumo huu haukuwa wa kufurahisha wanasiasa mbali ulinuiwa kupeleka maendeleo mashinani na manufaa yake yameonekana katika muda mfupi.

Kuumbua muundo huu wa utawala ili kuridhisha wanasiasa wachache hakuwezi kuwa sehemu ya kuunganisha Wakenya.

Kwa maoni yangu, pendekezo lisilokuwa la kutia nguvu mfumo wa ugatuzi ulivyo kwa wakati huu halifai kuwepo katika ripoti ya BBI ikiwa kweli ililenga kuunganisha Wakenya.

Japo ninaunga mfumo wa serikali ambao utashirikisha Wakenya wote, ninahisi kuwa kubuni vyeo zaidi hakutasuluhisha tatizo la muda mrefu la ukosefu wa ushirikishi na usawa serikalini.

Hii ni kwa sababu wanasiasa huwa wanateua washirika na vibaraka wao badala ya Wakenya waliohitimu bila kujali wanakotoka.

Ni kawaida ya viongozi kuwapuuza Wakenya wanaohitimu kwa kazi muhimu na kuteua vibaraka wao wa kisiasa ambao hawajahitimu. Njia ya pekee ya kuhakikisha ushirikishi ni kukumbatia uzalendo kwa upana wake, uadilifu na kufuata sheria ambazo viongozi wamekuwa wakipuuza na kuzidharau.

Hata tukibadilisha katiba yote itakuwa ni kazi bure ikiwa badala ya kuitekeleza kikamilifu itatekelezwa kufaidi wachache walio na ushawishi ili waweze kukadamiza wengi wanaosingizia inalenga kuwafaidi.

Kumekuwa na madai kwamba mapendekezo ya BBI yanalenga pia kuleta usawa. Kwa maoni yangu, usawa nchini unaweza kupatikana kupitia ugavi wa mapato ambao utahakikisha kila eneo linapata maendeleo na sio kubuni vyeo vitakavyowafaidi wanasiasa.

Kauli zote zinazotolewa kuhusu BBI ni sawa na msemo maarufu wa danganya toto, huku wanasiasa wakilenga kufumba macho raia waendelee kujitafutia vyeo.

Wakenya wanaweza kuungana wanasiasa wakikoma kuhubiri ukabila, wakiacha kutoa matamshi ya chuki na uchochezi.

Wakenya wanaweza kuungana wanasiasa wakihuburi undugu wa dhati, naserikali ikiongozwa na sheria badala ya tamaa ya viongozi. Wakenya wanaweza kuungana na kuishi kwa amani kabla, kwenye uchaguzi na baada ya uchaguzi ikiwa utakuwa huru haki na kufanywa kwa uwazi.

Tukatae wito wa kuumbua Katiba kwa kisingizio cha kujenga uwiano ili kufaidi wachache wanaotaka tuwe watumwa wa wanasiasa.