Makala

MATHEKA: Heko kwa maafisa wetu wa polisi kwa kazi murua

February 19th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

IWAPO kuna kitu kilichonifurahisha wiki iliyopita, ni utendakazi wa maafisa wa polisi.

Ninajua kwamba huwa wanafanya mengi katika kazi yao ya kudumisha usalama kwa wote na haikuwa tofauti na wiki jana.

Hata hivyo, ninataka kutaja matukio matatu ambayo yalinifanya kuwaonea fahari maafisa wetu wa polisi na nitaeleza ni kwa nini. Kwanza, wiki iliyopita ilianza kwa ripoti kuhusu kutoweka kwa mwanaharakati Carole Mwatha mtaani Dandora, Nairobi.

Hofu ya wengi ilikuwa kwamba mwanaharakati huyo ambaye mwili wake ulipatikana katika mochari ya City baada ya siku sita, alikuwa ametekwa nyara na kuuawa kwa sababu ya kulaumu polisi kwa mauaji ya kiholela mtaani humo.

Kwenye mitandao ya kijamii, polisi walirushiwa kila aina ya lawama, watu wakasahau kwamba wanawahitaji kwa usalama wao kila siku.

Kile ambacho raia hawakufahamu ni kwamba wapelelezi walikuwa wakifanya kazi yao kwa kufuatilia simu ya mwanaharakati huyo hadi wakagundua kwamba alikuwa katika hospitali moja mtaani humo na sababu ilikuwa ni kujaribu kutoa mimba.

Cha kusikitisha ni kuwa polisi wasingemuokoa kwa sababu wakati walipopata habari kuhusu kutoweka kwake, alikuwa ameaga dunia.

Licha ya lawama za kila aina, kutoka kwa raia na makataa kutoka kwa wanaharakati, polisi walifanya kazi yao na kuwakamata washukiwa na kuwafikisha kortini kwa wakati.

Joto lilitulia upasuaji wa maiti uliofanywa na mwanapatholojia huru kuthibitisha kwamba mwanaharakati huyo aliaga dunia akijaribu kutoa mimba.

Polisi walibeba lawama lakini walidumisha utaalamu wa hali ya juu kuchunguza mauaji hayo na wanafaa kupongezwa. Naomba kumpongeza kiongozi wa uchunguzi huo, Inspekta Mkuu Joseph Wanjohi wa ofisi ya upelelezi ya Dandora kwa ustadi, utulivu na utaalamu wake katika uchunguzi wa kutoweka na mauaji ya Bi Mwatha.

Funzo

Hapa kuna funzo kwa Wakenya kwamba wanafaa kuwa na subira na kuwapa maafisa wa usalama nafasi ya kufanya kazi yao. Muhimu kwa umma ni kushirikiana na polisi kwa kutoa habari muhimu badala ya lawama.

Aidha, ni wiki jana ambapo aliyekuwa afisa wa cheo cha juu alihukumiwa kunyongwa kwa mauaji, ishara kwamba sheria ikifuatwa kikamilifu haki itatendeka kwa wote.

Katika kisa kingine, Kaunti ya Nyeri wiki jana, polisi walimtia mbaroni mshukiwa wa kujitoa mhanga akielekea katika chuo kimoja kikuu na kumpata na vifaa vilivyoshukiwa kuwa vilipuzi.

Najua kwamba polisi wamefaulu kuzima mashambulio mengi lakini ninahisi kukamatwa kwa mshukiwa huyu huenda kulizuia hasara kubwa hasa ikikumbukwa mkasa wa chuo kikuu cha Garissa.

Tukio jingine ambalo polisi walidhihirisha ustadi wao wiki jana ni kumsaka na kumkamata mshukiwa aliyekuwa akijifanya chokoraa. Picha ya mhalifu huyo iliposambazwa katika mitandao ya kijamii akiwa na bastola, polisi walichukua hatua za haraka na kumnasa.

Hili ni funzo kwa Wakenya kwamba wakitoa habari za kuaminika kwa polisi, visa vya uhalifu vinaweza kukabiliwa vilivyo.