Makala

MATHEKA: Huu si wakati ufaao kwa Haji, Kinoti kuumbuana

March 10th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Ni muhimu kusema ukweli ikiwa vita dhidi ya ufisadi ambavyo vimevumishwa mno katika kipindi cha pili cha utawala wa Rais Uhuru Kenyatta vitafaulu.

Nasema hivi nikijua kwamba ufisadi hufanya wanaouendeleza kuwa matajiri na wanatumia utajiri huo kulemaza vita dhidi ya uovu huu ambao ni adui wa taifa.

Hata hivyo, kilichoteka hisia zangu ni uhusiano kati ya afisi mbili muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya ufisadi kuonekana kuvurugika.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) George Kinoti na mwenzake wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji wamelaumiana hadharani kuhusu majukumu yao.

DCI analaumu DPP kwa kulemaza vita hivi akidai amekataa kutoa mwelekeo anapokabidhiwa faili za uchunguzi wa madai ya ufisadi.

Naye DPP analaumu DCI kwa kufanya uchunguzi duni unaofanya kesi kutofaulu mahakamani. Kulingana na DCI, waendesha mashtaka wameshindwa kuendesha kesi vyema na kufanya washukiwa kuachiliwa huru na mahakama.

Haya yote yalijitokeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Daniel Manduku alipoachiliwa idara hizo mbili zilipokosa kuelewana. DPP alidai hakuwa ameidhinisha mashtaka licha ya Bw Manduku kufikishwa kortini huku DCI akiwasilisha karatasi ya mashtaka ambayo haikuwa imepitia kwa DPP.

Kwa kuwa ni DPP anayepaswa kuidhinisha mashtaka na hakuwa amefanya hivyo, mahakama haikuwa na budi kumwachilia Bw Manduku. Kulingana na tajiriba niliyo nayo katika mfumo wa haki, idara hizo mbili zinastahili kuacha kulaumiana hadharani. Kila moja inafaa kutambua na kukubali udhaifu wake na kuurekebisha ikiwa vita dhidi ya ufisadi vitafaulu.

Ni jukumu la DCI kuchunguza kesi na uchunguzi usipokuwa wa kina, DPP, ambaye jukumu lake ni kuidhinisha mashtaka na kuyaongoza kortini, hawezi kuthibitisha kesi kortini.

Idara hizo mbili zikikosa kushirikiana na kila moja kutekeleza majukumu yake kikamilifu bila shaka, vita dhidi ya ufisadi havitafaulu na wafisadi watapata nguvu ya kuendelea kupora mali ya umma.

Ni kweli baadhi ya waendesha mashtaka hawana uzoefu wa mawakili wanaotetea washukiwa. Ni kweli kuwa baadhi ya wapelelezi huwa wanaacha habari muhimu katika uchunguzi zinazoweza kulemaza kesi. Ni kweli kuwa, ni kazi ya DPP kuchunguza kila faili anayopata kutoka kwa DCI ili kuridhika kuwa uchunguzi unatosha kufanikisha kesi kortini.

Pia, ni kweli kuwa, washukiwa wanaweza kufanya lolote kusambaratisha kesi zao wakati wa uchunguzi au wakati wa mashtaka na kwa hivyo ni ushirikiano wa dhati kati ya idara hizi mbili unaoweza kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.

Kama nilivyotangulia kusema, ni ukweli na nia njema zitakazofanya vita hivi kufanikiwa.

Ninahisi kuwa huenda mawasiliano kati ya afisi hizi mbili yamevunjika na ndicho chanzo cha mzozo wa sasa.

Kuvunjika kwa ushirikiano huu ni ushindi kwa washukiwa wa ufisadi na makuhani wa ufisadi ambao hawakufurahia jinsi wawili hao walijitolea kuangamiza uovu huu.

Ikizingatiwa kuwa washukiwa wa ufisadi huwa na watu wenye ushawishi serikalini, sio ajabu kuna watu wanaokosanisha wawil hao ili kulemaza vita hivi.