Makala

MATHEKA: Idara husika ziwe na azma moja ya kumaliza ufisadi

January 15th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusu kesi za ufisadi nchini. Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na mwenzake wa upelelezi wa jinai (DCI) George Kinoti wanaamini kwamba wamefanya kazi yao vyema kwa kuchunguza, kuwakamata washukiwa na kuwafungulia mashtaka.

Kufikia sasa, inaonekana kuwa wamefaulu kuwanasa samaki wakubwa na kuvunja mitandao ya ufisadi katika mashirika kadhaa ya umma.

Hata hivyo, kufuatia kauli zao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, wanahisi kwamba juhudi zao zinalemazwa na mahakama.

Sio mara moja Bw Haji amelaumu mahakama kwa kuachilia washukiwa wa ufisadi na kuwaruhusu kurejea kazini katika ofisi za mashirika ambayo huwa wamelaumiwa kusimamia vibaya au kuzitumia kupora mali ya umma.

Kwa mtu asiyeelewa sheria, madai haya yanaonekana ya kweli. Hata hivyo, kulingana na sheria, kila mshtakiwa, naam, kila mshtakiwa, ana haki ya kuachiliwa kwa dhamana nafuu bila kujali makosa yanayomkabili.

Sheria inasema mshukiwa anaweza kunyimwa dhamana tu upande wa mashtaka ukiwasilisha sababu za kutosha kuridhisha mahakama kwamba hataweza kufika kortini wakati wa kusikilizwa kwa kesi.

Kumekuwa na mjadala kuhusu sababu zinazofaa kuwa za kutosha na kuridhisha kufanya mshtakiwa kunyimwa dhamana, suala ambalo linafaa kushughulikiwa kikamilifu na wanaohusika na kutunga au kurekebisha sheria.

Kazi ya mahakama ambayo imebebeshwa lawama kwa kuwaachilia washukiwa licha ya upande wa mashtaka kuomba wanyimwe dhamana sio kutunga sheria, ni kuzitafsiri kwa muktadha wa ushahidi unaowasilishwa na kila upande.

Sisemi kwamba mahakama zetu hazina udhaifu, hapana, ninafahamu kuna mengi yanayohitaji kufanywa kuhakikishia Wakenya wamepata haki bila kujali tabaka lao katika jamii.

Ninachosema ni kwamba badala ya kurushiana lawama katika mitandao ya kijamii, kwenye vyombo vya habari na mikutano ya kijamii, wakuu wa idara husika wanafaa kutafuta mbinu za kurekebisha hali bila kusahau kwamba kila mshtakiwa ana haki zake.

Kwa mfano, ni nini kinachozuia Rais Uhuru Kenyatta kuandaa kikao na Jaji Mkuu David Maraga, Spika wa bunge Justin Muturi na mwenzake wa seneti Kenneth Lusaka kujadili kwa nia njema, na kwa kuzingatia haki za binadamu, jinsi ya kufanikisha vita dhidi ya ufisadi?

Ninajua kuna uhuru wa mahakama ambao unafaa kulindwa lakini ninajua kwamba mihimili mitatu ya serikali inafaa kushauriana kwa heshima na bila kuingilia uhuru na majukumu ya mwingine.

Mihimili mitatu ya serikali inapolaumiana hadharani, kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi, kuwekeana masharti na makataa vita dhidi ya rushwa vitabaki kuwa ndoto.

Muhimu kabisa ni kwa uchunguzi wa kina ambao ninaamini asasi zetu zina uwezo wa kutekeleza, kuchanganua ushahidi, kuandaa mashtaka yanayofaa na kuwashtaki washukiwa kwa msingi wa ushahidi uliopo.

Ninaamini ushirikiano ukiwepo, ushahidi uwe wa kutosha na majaji wasipotumiwa kuyumbisha kesi, juhudi za sasa za kuangamiza rushwa zitazaa matunda.