MATHEKA: Kuongezeka kwa mapinduzi Afrika ni hatari kwa ustawi

MATHEKA: Kuongezeka kwa mapinduzi Afrika ni hatari kwa ustawi

Na BENSON MATHEKA

KUNA hatari ya hatua ambazo bara la Afrika limepiga katika kukuza demokrasia, kuporomoka kufuatia msururu wa mapinduzi ya kijeshi ya hivi majuzi katika nchi kadhaa.

Katika muda wa mwaka mmoja, wanajeshi wametwaa mamlaka katika nchi tatu kusini mwa jangwa la Sahara.

Wanajeshi wa kikosi maalumu walipindua serikali ya kiraia ya Mali ambapo Kanali Assim Goita alijitangaza rais.

Miezi michache baada ya Kanali Goita kuongoza mapinduzi Mali, wanajeshi walitwaa mamlaka Chad baada ya kifo cha Rais Iddris Derby.

Mwanawe Derby, Jenerali Mahamat Derby alitangazwa rais wa nchi hiyo kwa usaidizi wa Ufaransa iliyotawala nchi hiyo enzi za ukoloni.

Mapema mwezi huu Septemba, Kanali Mamady Doumbouya aliongoza wanajeshi wa kikosi maalum, kupindua serikali ya kiraia ya Guinea na kumzuilia Rais Alpha Conde.

Mapema Jumanne, serikali ya mpito ya Sudan ilitangaza kuwa ilizima jaribio la mapinduzi mwaka mmoja baada ya kuondolewa mamlakani kwa Rais Omar el Bashir.

Msururu wa mapinduzi haya unazua kumbukumbu ya hali iliyokumba nchi kadhaa za kusini mwa jangwa la Sahara miaka ya kwanza baada ya kupata uhuru.

Wimbi la mapinduzi miaka ya sitini na sabini lilisababishwa na ukosefu wa usawa, utawala wa kiimla na wanajeshi vijana waliotaka kuonja mamlaka baada ya kupata mafunzo ng’ambo.

Watawala wa kijeshi waliua na kuwazuilia wapinzani wao, walikandamiza haki za raia wao, wakapora rasilimali na matokeo yakawa ni bara la Afrika kudumaa kimaendeleo.

Katika baadhi ya nchi hasa zilizo na utajiri wa madini na mafuta, mapinduzi yalichochewa na mataifa yenye nguvu yaliyotaka kuweka viongozi waliojali maslahi yao.

Katika miaka ya themanini, mapinduzi yalififia huku nchi nyingi za Afrika zikikumbatia demokrasia na kuruhusu raia kuchagua viongozi.

Wale walioingia mamlakani kupitia mapinduzi waliruhusu ushindani wa kisiasa kupitia uchaguzi na baadhi wakashinda na kuwa viongozi wa kiraia.

Kwa miaka ambayo demokrasia ilinawiri Afrika, bara hili lilipiga hatua kimaendeleo.

Raia walichangia katika ujenzi wa nchi zao, watoto walisoma na miundomisingi ikaimarika kwa sababu ya uthabiti wa kisiasa.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi walikwamilia mamlakani huku wakibadilisha katiba za nchi zao wapate kuendelea kutawala, kutumia mamlaka kuiba kura wakati wa uchaguzi na kukasirisha raia wengi ambao ni vijana wanaotaka mabadiliko.

Ingawa mapinduzi ya kijeshi si tiba ya utawala mbaya, si ajabu wanaoongoza mapinduzi hayo ni vijana wanaotwikwa majukumu ya kulinda nchi zao na marais wanaowapindua na si waasi wanaopigana msituni.

Kuzuka upya kwa mapinduzi ya kijeshi, kunaweza kurejesha Afrika enzi za giza kwa kufuta demokrasia na ustawi.

You can share this post!

WASONGA: Wabunge wapiganie kurejea kwa bei nafuu

Viongozi wa makanisa wataka bei ishuke