Makala

MATHEKA: Mageuzi yalenga kufanya raia watumwa wa serikali

September 9th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MKONDO ambao siasa zimechukua katika nchi hii, hasa tofauti kati ya Rais na Naibu Wake unaiweka katika hatari kuu.

Unaturejesha miaka michache baada ya Kenya kupata uhuru ambapo Rais Jomo Kenyatta alitofautiana na makamu wake Jaramogi Oginga Odinga. Tofauti zao zilisababisha uhasama wa kisiasa kati ya uliokuwa mkoa wa Nyanza na Magharibi na eneo la Mlima Kenya.

Mzozo baina yao ulipelekea mabadiliko ya kikatiba yaliyofanya wakosoaji wa serikali kutupwa kizuizini na hata kuuawa. Haya yamenukuliwa katika historia ya nchi hii. Maeneo waliyotoka waliokosoa serikali yalinyimwa maendeleo. Yalikosa barabara, shule na hospitali. Umasikini ulikita mizizi na watu kuteseka kwa sababu ya tofauti za kisiasa za viongozi. Sio siri kwamba, ni siasa za wakati huo zilizokuza ukabila ambao umeendelea kuwa donda katika nchi hii.

Katiba ilibadilishwa kila wakati kutimiza maslahi ya viongozi binafsi na sio kwa manufaa ya raia. Mabadiliko kama hayo yalifanya Kenya nchi ya chama kimoja, Kanu, hatua ambayo ilipokonya raia haki na uhuru wa kujieleza, kukusanyika ili wasiweze kuungana kutetea haki zao. Ilichukua zaidi ya miaka 20 ya umwagikaji damu kupigania siasa za vyama vingi zilizoruhusiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa 1992.

Hata hivyo, ni katiba mpya iliyopitishwa 2010 ambayo ilipatia Wakenya matumaini. Kupitia katiba hiyo, waliamua jinsi wanavyotaka waongozwe. Walitoa mamlaka kwa asasi za serikali kuwaongoza na kwa muda wa miaka saba walifurahia katiba hiyo. Waliweza kujieleza, kukosoa serikali, kuandamana kwa amani na kuona haki za raia zikiheshimiwa.

Muhimu kabisa, Katiba hiyo iliwapa wakazi wa maeneo yaliyokuwa nyuma kimaendeleo matumaini kupitia ugatuzi. Masikini walipata matumaini huduma zilipopelekwa mashinani. Elimu msingi ikafanywa ya lazima kwa kila mtoto, miundo misingi ikaimarika pia na vituo vya afya vikajengwa katika kila kijiji kupitia ugatuzi.

Lakini sasa siasa zimechukua mkondo unaoweza kupokonya raia manufaa ya katiba hiyo. Viongozi wameungana kutaka ibadilishwe, hatua inayoweza kuwa tisho kwa ugatuzi. Sawa na ilivyokuwa baada ya uhuru, Rais na Naibu wake wametofautiana huku rais akitaka marekebisho ya kikatiba na naibu wake akiyapinga. Ukweli usemwe. Tofauti kati ya viongozi hawa sio dalili nzuri kwa nchi.

Tumeona juhudi za wanasiasa za kurejesha nchi katika utawala wa chama kimoja kwa kufifisha upinzani ndani na nje ya bunge. Hata kabla ya Katiba kurekebishwa, tumeona polisi wakitumiwa kuwakamata watu kwa kutoa maoni yanayotofautiana na ya viongozi wa serikali.

Katika miaka kumi ya utawala wa Rais Mwai Kibaki ambao Kenya ilifikia kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi, tulishuhudia demokrasia ikipanuka. Raia na viongozi walikuwa na uhuru wa kukosoa serikali bila kuogopa kutiwa mbaroni. Serikali ilikuwa ya kutumikia watu, haikuwa ya watu kulazimishwa kuitumikia.

Kama mkondo huu ungedumishwa chini ya katiba ya 2010 ambayo kwa hakika inatoa mwongozo wa kufanya hivyo, Kenya ingekuwa imefikia ustawi wa hali ya juu. Mkondo wa siasa ambao uko kwa sasa na unaokusudiwa, unalenga kufanya raia watumwa wa serikali.