MakalaSiasa

MATHEKA: Mikutano ya wanasiasa kuhusu BBI haifaidi raia

February 16th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Nimekuwa nikifuatilia mikutano ya kimaeneo ya kuvumisha ripoti ya mpango wa maridhiano maarufu kama BBI.

Tayari mikutano minne imefanyika na wa tano unatarajiwa kaunti ya Meru Februari 29.

Mkutano wa kwanza ulifanyika Kisii na kuhudhuriwa na wanasiasa wa vyama tofauti na viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri.

Mkutano wa pili ulikuwa Kakamega na vilevile ulihudhuriwa na wanasiasa wa vyama tofauti na viongozi wa serikali.

Mikutano sawa ilifanyika Mombasa na Kitui ambapo viongozi waliwasilisha mapendekezo kuhusu masuala wanayohisi yatafaidi eneo lao yakijumuishwa katika BBI.

Katika kila eneo, mikutano hiyo ilikuwa ikitanguliwa na kongamano la viongozi wa eneo husika kujadili na kupitisha maazimio yao.

Kabla ya kila mkutano, viongozi walikuwa wakifanya kampeni kali ili wakazi wahudhurie kwa wingi. Kwa maoni yangu, mikutano hii ni ya kupoteza wakati ikiwa kweli lengo ni kuhamasisha wakazi kuhusu BBI.

Nguvu, muda na pesa zinazotumiwa kuandaa mikutano hiyo zinaweza kutumiwa kwa masuala mengine muhimu kwa ujenzi wa taifa.

Ninasema hivi kwa sababu hakuna kipya kinachotoka kwa mikutano hiyo. Mikutano ninayounga, na inayofaa kuwa mara kwa mara, na huwa inafanyika hata kabla ya BBI, ni ya viongozi wa maeneo kwa lengo la kujadili uchumi, maendeleo na usalama. Mikutano ya viongozi wa kila eneo inatosha kujadili mahitaji ya wakazi na kuandaa maazimio ya kuwasilisha kwa jopokazi lililopatiwa jukumu la kufanikisha mchakato wa maridhiano.

Inashangaza kwamba ingawa imebatizwa jina la mikutano ya kuhamasisha wakazi kuhusu BBI, hakuna kinachofanyika isipokuwa kusoma maazimio, kucheza reggae, kuumbuana na kutawanyika.

Ninaamini kwamba jopokazi lililoandaa ripoti ya BBI ina uwezo wa kutekeleza majukumu yake na wa kufika kila eneo kukusanya maoni au kupokea maazimio. Hii ya kucheza reggae inatagawanya Wakenya zaidi.

Ikiwa mchakato wa BBI ni wa kuunganisha Wakenya kwa roho safi, basi mikutano hii inapaswa kusitishwa na kuachia kamati inayoongozwa na Seneta Yusufu Haji kuushughulikia.

Ninashuku kuwa wanasiasa wanataka kutumia mikutano ya kimaeneo wanayofanya kuteka mchakato huo kwa lengo la kutimiza malengo yao ya kibinafsi.

Kusitisha mikutano hii kutapatia jopokazi fursa ya kupokea maoni moja kwa moja kutoka kwa wananchi kinyume na inavyofanyika katika mikutano hiyo.

Wanachotaka wanasiasa, ni kutumia mikutano hiyo kujivumisha ili mazingira ya kisiasa yakibadilika wasijipate kwenye baridi. Hii inajitokeza wazi katika kila mkutano ambapo viongozi huwa wanamkabidhi kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, maazimio ya eneo lao.

Akiwa mmoja wa waasisi wa mchakato huu na aliyeunda jopokazi la Seneta Haji na ikiwa ana nia njema katika BBI kwa Wakenya, Bw Odinga anapaswa kugundua kuwa mikutano hii haitendei haki mpango huu.

Mfano mzuri ni kutoridhishwa kwa baadhi ya wabunge na jinsi mikutano hiyo inavyoandaliwa na jaribio la wandani wa naibu rais William Ruto kupanga mikutano zaidi.

Jopo la Bw Haji lina hadi Juni kukamilisha kazi yake, limetambuliwa kwa kuwa limechapishwa katika toleo maalumu la gazeti rasmi la serikali inavyohitajika kisheria tofauti na mikutano ya wanasiasa.