MATHEKA: Miungano mipya ya kisiasa isiwe ya kupiganisha raia

MATHEKA: Miungano mipya ya kisiasa isiwe ya kupiganisha raia

Na BENSON MATHEKA

HUKU miungano ya kisiasa ikiendelea kusukwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, kuna hatari ambayo Wakenya wanafaa kuwa chonjo wasitumbukizwe na wanasaisa kwenye machafuko.

Kwa kawaida uchaguzi mkuu unapokaribia, wanasiasa huwagawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila na kutumia miungano ya kisiasa kuchochea ghasia.

Ni hali hii iliyosababisha ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo watu zaidi ya 1,300 waliuawa na zaidi ya 600,000 wakafurushwa makwao.

Ingawa ghasia hizo zilitokea baada ya uchaguzi, zilikuwa matokeo ya matamshi ya chuki na uhasama ambao wanasiasa walikuwa wamepanda wakati wa kampeni.

Hali hiyo imeanza kujitokeza tena huku baadhi ya wanasiasa wakisemekana kupanga miungano ambayo wanatumia jamii zao kujipigia debe.

Baadhi yao wamesikikika wakiwa na misimamo mikali wakisema jamii za eneo fulani haziwezi kuunga mkono wagombeaji urais kutoka maeneo fulani.

Kauli hizo zinaashiria wako tayari kuchochea jamii wanazotoka dhidi ya jamii zingine na hii ndiyo hatari ambayo raia wanafaa kuepuka.

Wakati ghasia za kisiasa zinapotokea, ni raia wa kawaida wanaoteseka na sio viongozi wa kisiasa wanaowafanya wapigane.

Wakati raia wanapopigana, wanasiasa huwa wanaketi na kujadili jinsi ya kugawana mamlaka waweze kuwatawala.Wanapoingia mamlakani, huwa wanawasahau waliopigana.

Hakika, wanachofanya wanasiasa wanapoingia mamlakani ni kupora mali ya umma badala ya kuitumia kuboresha maisha ya raia.

Hapa kuna funzo kwamba wanasiasa huwa wanatumia raia masikini kutimiza maslahi yao ya kibinafsi huku wakiwapatia ahadi feki.

Hivyo basi, wakati huu ambao wanasiasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, raia wanafaa kuwa chonjo ili kuepuka kutumbukizwa katika ghasia kama miaka iliyotangulia.

Hii inawezekana ikiwa Wakenya watazinduka na kukataa miungano yoyote inayoegemea ukabila.

Kulingana na tajiriba ya chaguzi zilizopita hasa wakati wa kipindi cha mpito rais mmoja anapokabidhi mwingine mamlaka itakavyofanyika kwenye uchaguzi mkuu ujao, ipo haja ya Wakenya kubaini kwamba wanasiasa huwa wanatumia jamii zao kama ngazi ya kutwaa uongozi.

Wakifaulu kuingia mamlakani, vijana wanabaki bila kazi, hospitali zinakosa dawa, ushuru unapanda na bei za bidhaa kuongezeka huku wanasiasa na familia zao wakila, kuteremsha na kusaza.

Wakenya wakikataa kuchochewa na wanasaisa, watakuwa wamebadilisha mazingira ya siasa za uchaguzi humu nchini. Miungano ya kisiasa inafaa kuwa ya kuunganisha Wakenya kwa nia njema na sio ya kuwagawanya.

You can share this post!

Hatuhitaji Haaland na hatuna mpango wa kuuza Lewandowski...

WASONGA: EACC itaje wazi watumishi wa umma wachapao siasa