Makala

MATHEKA: Serikali ilipe wahudumu wa afya kuokoa Wakenya

August 24th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KILIO kimetanda kote nchini madaktari na wahudumu wa afya wa viwango tofauti wakigoma wakitaka mazingira bora ya kazi wakati huu wanapopambana na janga la virusi hatari vya corona.

Ni kilio cha wahudumu hao wakitaka haki, na cha wagonjwa wakitaka huduma zao. Kufikia sasa, wahudumu wa afya 15 wamepoteza maisha yao kutokana na virusi hivi na zaidi ya 900 wameambukizwa.

Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha kutetea maslahi ya madaktari Dkt Chibanzi Mwachonda mmoja wa walioambukizwa virusi hivyo alisema kwamba alivipata akitekeleza majukumu yake kama daktari.

Japo wahudumu wa afya, sawa na Wakenya wengine wanaweza kuambukizwa wakiwa mahali popote, ukweli ni kwamba wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa wakiwa kazini kwa kuwa wanatangamana na wagonjwa, wengi ambao, kulingana na wizara ya afya, hawana dalili za ugonjwa huu.

Hivyo basi, wanapolaumu wizara ya afya na serikali za kaunti kwa masaibu yao, wako na kila sababu ya kufanya hivyo.

Wameanza kugoma katika kaunti nyingi hatua ambayo bila shaka itatumbukiza nchi katika hatari kubwa wakati huu wa janga hili linalohangaisha ulimwengu.

Tumeona wagonjwa wakihangaika bila wa kuwahudumia katika hospitali kote nchini wahudumu wa afya walipogoma awali.

Tulishuhudia pia wagonjwa wakifariki kwa kukosa matabibu wa kuwahudumia. Inasikitisha basi, serikali haikujifunza kutoka migomo ya awali ya wahudumu wa afya.

Inasikitisha wakati huu ambao huduma za madaktari, wauguzi, matabibu na wataalamu wa maabara zinahitajika zaidi kusaidia wagonjwa wakati huu wa janga hatari serikali inaweza kuwapuuza kwa kutowalipa mishahara yao.

Hata kama afya ni huduma iliyogatuliwa na kaunti hazijatumiwa pesa kutokana na mzozo kuhusu mfumo wa ugavi wa pesa za kaunti katika seneti, haimaanishi zimefilisika kiasi cha kutowalipa wahudumu wa afya na kuhakikisha wanapata vifaa bora vya kazi kuwakinga dhidi ya kuambukizwa maradhi.

Mbali na kutolipwa mishahara wanachosema ni kuwa wanahitaji vifaa bora sio bora vifaa wizara ya afya inavyoamini inaposema imesambaza vifaa vya kutosha kwa hospitali zote kote nchini.

Ikizingatiwa kwamba nchi hii ina uhaba wa wahudumu wa afya na mfumo hafifu wa afya, mgomo wa wahudumu hao wakati huu huduma zao zinapohitajika kukabiliana na janga la corona unaweza kusababisha hasara kubwa.

Ni haki ya wahudumu wa afya kugoma sawa na ilivyo haki ya serikali kuwalipa mishahara kila mwezi. Ni haki ya serikali kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata haki ya huduma bora za afya na ni haki ya Wakenya kudai haki hii kutoka kwa serikali.

Kwa hivyo, serikali haina budi kutekeleza jukumu lake kwa wahudumu wa afya na Wakenya. Migomo ya kila mara ya wahudumu wa afya inaonyesha kuwa serikali imeshindwa kutekeleza jukumu lake ipasavyo.

Matokeo ni Wakenya kufariki kwa kukosa huduma za afya.

Ukweli mchungu ni kuwa huku wahudumu wa afya wakikosa mishahara na vifaa bora vya kazi, mabilioni ya pesa na vifaa vilivyotolewa na wafadhili kuwasaidia katika vita dhidi ya corona viliporwa na watu wenye ushawishi serikalini baadhi yao wanaowashutumu kwa kugoma au wanaowashawishi kurudi kazini.

Tunahitaji kuwalinda wahudumu wa afya ikiwa tunajali maisha ya Wakenya wakati huu wa janga la corona.