Makala

MATHEKA: Suala la umri wa kushiriki ngono lijadiliwe kwa makini

April 2nd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MJADALA ambao umekuwa ukiendelea tangu majaji wa Mahakama ya Rufaa walipopendekeza umri wa wasichana kukubali kwa hiari kufanya mapenzi upunguzwe unafaa kuendeshwa kwa uangalifu.

Japo baadhi ya watu hasa wanasiasa waliingiza siasa katika pendekezo hilo ninaamini majaji hao walikuwa na sababu ya kulitoa.

Wakiwa na tajriba pana katika masuala ya kisheria hasa ikizingatiwa kuwa ili kuhitimu kuwa jaji mtu anafaa kuwa mwanasheria aliyehudumu kwa miaka 15, nina sababu ya kusadiki kwamba pendekezo lao halikuwa la kubahatisha.

Mbali na kuwa waamuzi katika masuala ya haki, majaji hao ni wazazi, na sehemu ya jamii tunayoishi. Baadhi yao wana watoto wasichana na wanaelewa mabadiliko yaliyopo kitabia katika kizazi cha sasa.

Ulimwengu umebadilika pakubwa na hatuwezi kufumbia macho ukweli wa mambo.

Kulingana na majaji hao, kuna watu wanaoozea jela kwa sababu ya kufanya mapenzi na wasichana ambao walikubali kwa hiari yao kushiriki tendo hilo. Makosa waliyofanya wafungwa hao ni kuvunja sheria kwa kushiriki mapenzi au kuhusisha wasichana walio na umri mdogo katika kitendo cha aibu.

Hii ni kwa sababu sheria inavyosema kwa sasa ni kuwa mtu yeyote ambaye hajatimiza umri wa miaka 18 ni mtoto.

Pendekezo la majaji ni kuwa sheria inafaa kubadilishwa ili umri wa msichana au mwanamume kufanya uamuzi wa kushiriki mapenzi uwe miaka 16.

Hii pia itafaidi wanawake ambao wamekuwa wakifungwa jela kwa kufanya mapenzi na wavulana walio na umri wa chini ya miaka 18. Katika kisa kimoja mwaka jana, mahakama moja nchini ilikataa utetezi wa mwanamke aliyeshtakiwa kwa kufanya mapenzi na mvulana wa umri mdogo aliposoma ni mvulana huyo aliyemtongoza na alionekana kuwa mtu mzima walipokutana katika kilabu.

Kwa vile mvulana alikuwa na umri mdogo, mahakama ilimfunga jela kwa kumshirikisha mtoto katika kitendo cha ndoa. Wadadisi wa masuala ya sheria walikubaliana kuwa jaji hakuweza kumwachilia mwanamke huyo kwa sababu kwa kufanya hivyo, hangekuwa akifuata sheria ambayo ni msumeno hukata kuwili.

Ninasadiki kuwa lengo la majaji waliotoa pendekezo la kupunguza umri wa mtu kutoa uamuzi wa kufanya mapenzi kwa hiari halikuwa kulinda mababu wanaodhulumu watoto wa rika la wajukuu wao baadhi ya watu wanavyodai.

Nina hakika wanafahamu kwamba katika umri wa miaka 16 wasichana wengi huwa katika kidato cha tatu au cha nne na wengine darasa la nane kwa kutegemea wanakotoka.

Nina hakika wanafahamu kwamba kuna walimu na viongozi wa kidini ambao wamekuwa wakiwadhulumu kimapenzi watoto wanaopaswa kuwalinda.

Nina hakika kwamba majaji hawakunuia kulinda walimu wanaotafuna wanafunzi wao kwa kisingizio kwamba wako na umri unaofaa kufanya uamuzi.

Nina hakika wanaelewa mazingira ambayo wasichana wamekuwa wakipitia kwa kuozwa mapema kwa sababu ya umaskini.

Mjadala huu, unafaa kufanywa kwa uangalifu na kama kuna hatua zitakazochukuliwa ziwe za kulinda wasichana wetu.