Matiang’i aahidi kuanika walanguzi wa mihadarati

Matiang’i aahidi kuanika walanguzi wa mihadarati

Na MOHAMED AHMED

WAZIRI wa Usalama wa Kitaifa, Dkt Fred Matiang’i amefichua mipango ya serikali ya kuchapisha majina ya walanguzi wa dawa za kulevya humu nchini.Akizungumza jijini Mombasa baada ya kukutana na viongozi wa mashinani katika ukumbi wa Tononoka, Dkt Matiang’i alisema mipango hiyo inaendelea.

“Nitahakikisha kuwa ahadi niliyoweka inatimia. Kwa sasa mipango bado inaendelea kwa sababu tunapaswa kufanya mambo yote kisheria,” akasema Dkt Matiang’i.

Mwaka jana, Dkt Matiang’i alikuwa ameahidi kuwa serikali itachapisha majina ya wanafanyabiashara wanaohusika katika biashara hiyo ya ulanguzi wa dawa za kulevya pamoja na majina ya biashara ambazo wamekuwa wakizitumia kuficha biashara zao haramu.

Mpango huo unalenga kupambana na wakuu wa ulanguzi wa dawa za kulevya hususan wale ambao wamekita mizizi katika ukanda wa Pwani.

“Mliona kabla ya Krismasi mwaka jana tulichapisha majina ya wale wanaohusika kuwafadhili washukiwa wa ugaidi na hivyo ndivyo tutakavyofanya kuhusiana na wale wanaohusika katika ulanguzi wa dawa za kulevya,” akasema.

Alisema serikali haitaruhusu watu wachache kuendela kunufaika huku mamia wakiendelea kuteseka kwa sababu ya biashara hiyo haramu.

Dkt Matiang’i aliongea jana saa kadhaa baada ya washukiwa wanne wa ulanguzi wa dawa za kulevya kukamatwa na kilo mbili za heroini yenye thamani ya Sh6 milioni.

Miongoni mwa waliokamatwa ni mume na mke raia wa Tanzania na watu wengine wawili ambao walikamatwa eneo la Mombasa. Maafisa wa polisi waliovamia nyumba walikoshikwa wawili hao walikuwa wamelenga mlanguzi wa dawa za kulevya ambaye alikuwa anatumia dawa hizo eneo la Lamu.

Wakati huo huo, Dkt Matiang’i alisema kuwa anaunga mkono mpango wa kupitisha mswada ambao utabuni adhabu kali kwa walanguzi wa dawa za kulevya.

Aidha, Dkt Matiang’i alitembelea miradi tofauti ya serikali ikiwemo ule wa daraja la kuelea la Likoni na barabara ya Dongo Kundu.

Pia, alikutana na viongozi wa Kiislamu ambapo aliwapa nakala za BBI na kuwasihi wapitie ripoti hiyo.Alisema kuwa serikali inalenga kuweka amani na umoja humu nchini na nikupitia BBI ndipo kutapatikana umoja huo.

Alisema kuwa mabadiliko yanayopendekezwa na BBI yanalenga kuleta manufaa kwa wananchi.

‘Kuna pesa zaidi zitakuja katika kaunti na pia kutakuwa na swala la kuunganisha Wakenya na kuhakikisha usawa wa kijamii na kijinsia na haya ni mambo muhimu kwetu sisi sote,” akasema Dkt Matiang’i.

Alisema ni kupitia umoja wa wananchi ndipo nchi ya Kenya itasonga mbele. Alisema suala la BBI silo la kulazimishwa mtu kwa sababu Kenya ni nchi huru na kila mmoja ana uhuru wake.

You can share this post!

Waziri motoni kukodisha choo kwa Sh2.3m

Uangalizi mdogo, mahitaji machache msukumo tosha wa kukuza...