Habari

Matiang'i aamuru MCAs wapokonywe bunduki

July 30th, 2020 1 min read

Na MARY WAMBUI

MAKABILIANO ya mara kwa mara kwenye bunge la Kaunti ya Nairobi, sasa yamemsukuma Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kuagiza MCAs wote wapokonywe bunduki.

Dkt Matiang’i pia ameagiza leseni za madiwani wote wanaomiliki bunduki zifutiliwe mbali, na kusema hatua sawa na hiyo itachukuliwa dhidi ya madiwani wengine kitaifa wanaokosa nidhamu.

Mnamo Jumanne, vita vikali vilichacha kwenye majengo ya bunge hilo ambapo polisi walinaswa kwenye kamera wakimchapa vikali diwani wa Mlango Kubwa, Patricia Mutheu. Ghasia hizo zilizuka baada ya sehemu ya madiwani kujaribu kumfikia spika Beatrice Elachi kwa lengo la kumkabidhi nakala ya notisi ya kumtimua mamlakani.

Dkt Matiang’i alitaja Bunge la Kaunti ya Nairobi kama ngome ya vita ambapo madiwani huamua kupigana badala ya kujadiliana.

Alisisitiza kwamba, wawakilishi wadi wenye mazoea ya kutumia ghasia hawafai kuendelea kushikilia nafasi za uongozi kwa kuwa wanakiuka sura ya sita ya Katiba inayozungumza kuhusu uongozi na uadilifu.

“Tumechoka kuishi katika hali hii ya vurugu zisizokamilika kila mara. Kile ambacho hutokea kwenye bunge hilo ni matendo ya uhalifu na hatuwezi kuyavumilia zaidi. Lazima tukumbatie uamuzi wa kukomesha ghasia hizi ndiyo maana sasa nimelazimika kutafuta mwongozo kutoka kwa Baraza la Kitaifa la Usalama kuhusu suala hili,” akasema Bw Matiang’i.

Alifichua kwamba, vita vya mara kwa mara kwenye bunge hilo vimelazimu serikali kuwatuma kati ya polisi 25-30 katika majengo hayo na maeneo ya karibu katikati mwa jiji.

“Tumechoka. Linalozua ghasia hizi ni ugomvi kuhusu uongozi. Haiwezekani kutumia kitengo cha usalama jijini kwa masuala yanayohusu Bunge la Kaunti ya Nairobi pekee,” akaongeza Bw Matiang’i.

Alisema kufikia sasa, kikosi chake cha usalama kimetwaa bunduki 14 ambazo zinatumika kutekeleza uhalifu wakati wa ghasia kati ya madiwani na wanaamini kuna nyingine zaidi ambazo wanalenga kunasa.

Katika ghasia za Jumanne, Bi Mutheu ambaye alipigwa na polisi aliwashutumu polisi kwa kumuadhibu vibaya badala ya kumkamata.