Habari Mseto

Matiang'i akaribishwa Migori kishujaa

July 27th, 2019 1 min read

Na RUTH MBULA , JOSIAH ODANGA na IAN BYRON

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i alipokewa Jumamosi kishujaa alipozuru eneo la Nyanza Kusini.

Viongozi walioandamana naye pia walimsifia, wakisema kuwa wako tayari kumuunga mkono kwa majukumu makubwa zaidi serikalini.

Waziri huyo aliwahimiza Wakenya kudumisha umoja, akisisitiza huu ni wakati wa kujenga nchi.

“Ninakubaliana na viongozi wetu kwamba huu ni wakati wa kufanya kazi. Ni muhimu kwetu kukumbuka kwamba sisi ndio tunaonufaika pakubwa na handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga,” alisema Matiang’i.

Alikuwa akihutubu katika Shule ya Msingi ya Kadika, Kaunti ya Migori, alikoongoza hafla ya kuchangisha fedha kusaidia Kanisa la Kiadventista (SDA) la Kadika.

Mamia ya washirika wa kanisa hilo kutoka Kongamano la Kiadventista la Ranen pia walihudhuria.

Mwenyeki wa ODM, Bw John Mbadi na Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Bw Junet Mohamed waliwaongoza wanasiasa wengine kumsifu Dkt Matiang’i kwa utendakazi wake bora katika kila wizara anakohudumu serikalini.

“Tangu ulipoteuliwa waziri, utendakazi wako umekuwa wa kuigwa. Umeitumikia nchi kwa ukakamavu mkubwa,” akasema Bw Mbadi.

Cheo

Bw Mbadi, ambaye pia ni mbunge wa Suba Kusini, alisema kuwa Dkt Matiang’i anastahili kupandishwa cheo kutokana na utendakazi wake.

“Unapofanya kazi vizuri, unatumaini kupandishwa ngazi. Kuna jambo linalokuja, ambapo litashirikisha watu watano na tuna hakika utakuwa hapo,” alisema.

Kwa upande wake, Junet alisema kuwa ingawa walitofautiana na waziri nyakati fulani awali, wao ni marafiki.

“Kwa sasa, fanya kazi kikamilifu kwa kushirikiana na Rais Kenyatta na Bw Odinga. Ikiwa kutaibuka nafasi yoyote baadaye, hatutakusahau,” alisema.

Gavana wa Migori Okoth Obado alisema kuwa anaunga mkono handisheki.

Viongozi waliokuwepo ni Seneta Ochillo Ayacko (Migori), wabunge Gladys Wanga (Homa Bay), Pamela Odhiambo (Migori), Janet Ong’era (Kisii) miongoni mwa wengine.