Makala

Matiang'i amzima Ruto kupata tenda ya sare za polisi

December 19th, 2018 2 min read

NA PETER MBURU

VITA baina ya waziri wa Usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i na naibu wa Rais William Ruto vinazidi kutokota japo bila yao kujitokeza moja kwa moja, waziri huyo akisemekana kumkanyagia breki Bw Ruto kutopata tenda za serikali.

Inadaiwa kuwa wakati Dkt Matiang’i alipolaumu ‘mtu fulani’ kuwa anawasukuma pamoja na Inpekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet na Katibu katika wizara yake Karanja Kibicho kumpa tenda ya kununua sare za polisi kutoka nje ya nchi, alikuwa akimrejelea naibu wa Rais.

Vita baina yao vinasemekana kuendelea kutokota, kwani japo Bw Ruto anasukuma kupewa tenda za serikali za mabilioni ya pesa pamoja na wandani wake, waziri huyo naye amekuwa akidinda, badala yake akichukua maamuzi ambayo yanamkera Bw Ruto.

Mkuu wa mawasiliano katika ofisi ya Bw Ruto, David Mugonyi hata hivyo amepinga madai hayo, akiyataja kuwa ‘upuzi’.

Lakini pia hali kuwa Dkt Matiangi amekuwa na uhusiano wa karibu na Rais Uhuru Kenyatta ni jambo ambalo haliwezi kupuuzwa katika vita hivyo.

Bw Ruto wiki hii anadaiwa kumtaka waziri huyo kupeana tenda ya kusambaza sare za polisi kwa watu wengine mbali na Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS), lakini akiongea kuhusu suala hilo Jumanne, waziri huyo alikuwa wazi na bila kujikanganya.

“Inspekta Jenerali, Katibu wa wizara pamoja nami tumekuwa tukisukumwa na baadhi ya walaghai tununue sare kutoka nje ya nchi. Nisikizeni kwa makini, hatutanunua sare za polisi kutoka nchi nyingine.

“Sasa wewe na wakora wako, mahali mlikubaliana mtaenda kununua sare utaenda uwaeleze hivi, hatutaenda kununua sare popote pengine. Ni rahisi hivyo tu,” akasema waziri huyo.

“Sharti tuinue viwanda vya nguo vya humu nchini. Tutasaidiaje wakulima wa pamba na watengenezaji katika viwanda na kuongeza nafasi za ajira bila kufanya hivyo? Kumekuwa na biashara ya gizani ambapo watu wanaenda mahali na kuelewana kununua sare kutoka nje ya nchi, kisha kutoa vijisababu kuwa viwanda vyetu havina uwezo,” aksema.

Vyombo vya ahbari Jumanne lilikuwa vimeripoti kuwa kuna upungufu wa vifaa vya kutengeneza sare hizo, ndiposa maafisa wa polisi bado hawajapokea.

Lakini waziri huyo alisisitiza kuwa zitatengenezewa humu nchini.

“Itakuwa na haja gani kwa serikali kuweka pesa kufufua kiwanda cha Rivatext ili kutoa nafasi za kazi Eldoret kisha kesho yake kama wajinga twende kununua sare za polisi kutoka mataifa ya nje kama vile Uturuki, China ama popote pale,” akauliza waziri huyo.

Vita baina ya viongozi hao wawili vinasemekana kuwa vimekuwa vikiendelea, siku chache zilizopita gavana mmoja kutoka eneo la Nyanza na ambaye ni mwandani wa Bw Ruto akisemekana kuwa alikuwa amewalipa watu kumpigia makelele waziri huyo akihutubu, kutokana na kuhangaishwa kwa wahudumu wa Bodaboda.

Dkt Matiang’i aliepuka mkutano huo.

Bw Ruto mnamo Jumatatu akiwa Kakamega alipinga oparesheni dhidi ya wahudumu wa Bodaboda, akisema kuwa wao ni wafanyabiashara kama wengine.

“Kuna wahudumu wengi wa Bodaboda Kenya na wao pia ni wafanyabiashara na nimewaambia wale wanaohusika wasiwatese watu wa Bodaboda,” akasema Ruto.

Viongozi hao wawili vilevile wanasemekana kukosana Februari mwaka huu kuhusiana na tenda ya mabilioni kuhusu ununuzi wa silaha.

Hii ilikuwa baada ya idara ya polisi kutangaza tenda ya Sh3bilioni ya kusambaziwa silaha. Baadaye Bw Boinnet aliandika barua kusema kuwa tenda hiyo ilipewa kampuni kutoka mashariki mwa Uropa lakini Dkt Matiang’i akakataa kuidhinisha.

Aidha, wawili hao wanasemekana kutofautiana vikubwa wakati Matiangi alipokuwa waziri wa elimu mnamo 2016, wakati viongozi wa bonde la ufa walivamia chuo kikuu cha Moi kumzuia Prof Laban Ayiro kuchukua wadhifa wa naibu chansela wa chuo hicho, baada ya Prof Richard Mibey kuondoka.

Bw Ruto anadaiwa kumtaka Dkt Matiang’i kumteua Prof Kosgey wa jamii ya Kalenjin lakini waziri huyo akakataa, akisisitiza kuwa Prof Ayiro ndiye alikuwa amefaulu zaidi kusimamia chuo hicho.