Habari

Matiang'i anatuonea bure, wadai baadhi ya wabunge kutoka Magharibi

January 23rd, 2020 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

BAADHI ya wabunge wa kutoka Magharibi sasa wanamlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i wakidai anaonyesha upendeleo katika kupeana maafisa wa kudumisha usalama kwa wanasiasa.

Wabuunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Justus Murunga (Matungu), Didmus Barasa (Kiminini) na aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa wamedai waziri Matiang’i anawalenga na kuwadhalilisha wanasiasa wanaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu.

Wakiongea katika hafla tofauti, wanasiasa hao walimtaka Matiang’i na Katibu katika Wizara Karanja Kibicho waonyeshe usawa bila upendeleo wowote hata ikitokea kwamba wanasiasa wanaunga ama upande huu au ule.

Bw Washiali amemtaka Matiang’i awaheshimu viongozi wa Jubilee waliompigia debe Rais Uhuru Kenyatta wakati akitafuta kuchaguliwa tena mwaka 2017.

“Tulifanya bidii kumpigia debe Rais Kenyatta na ni kutokana na juhudi zetu ambapo Matiang’i alifanikiwa kuteuliwa waziri naye Kibicho akafanikiwa kuwa katibu. Wanafaa kutuheshimu,” akasema Washiali.

Washiali aidha alisema hatarajii kwamba serikali waliokuwa wameweka imani kwayo inaweza ikawageuka ghafla.

Alikuwa akizungumza wakati wa kutoa maombi ya shukrani baada ya madai kwamba alikuwa ametoweka Jumamosi iliyopita ambapo alitarajiwa kuwaongoza baadhi ya viongozi wa Magharibi – wa mrengo wa Ruto – kuangazia masuala ya wakulima uwanjani Nabongo, Mumias.

Siku hiyo kulikuwa kumepangwa mkutano wa uhamasisho wa ripoti ya mchakato wa maridhiano (BBI) katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega; ikiwa ni umbali wa kilomita 40 kutoka Mumias.

“Mkutano wetu mwanzo tulikuwa tumeuratibu ufanyike Oktoba 2019, lakini tukasogeza hadi Januari 18, 2020, ambapo ilisadifu kwamba ule wa BBI ulikuwa unafanyika Kakamega. Maafisa waliotupa kibali Januari 8 nao tena waliruhusu kikundi cha vijana waliokuwa wameonyesha nia ya kuandaa maandamano mjini Mumias,” akaelezea Washiali.

Naye Bw Murunga alikosoa hatua ya polisi kwamba wataondoa walinzi wa waheshimiwa wanaokabiliwa na kesi akisema wanafaa kufurahia matunda yajayo na uongozi hadi pale itaamuliwe iwapo wako hatiani au la.

“Matunda yajayo na uongozi yanalindwa na Tume ya Huduma za Bunge na hivyo kuwanyima wabunge haki ya kuwa na walinzi inakiuka Katiba. Tusiingize siasa kwa suala la ulinzi na usalama wa viongozi,” akasema Murunga.

Walisema kwamba mkutano wao utaandaliwa Januari 25 katika uwanja wa Nabongo ambapo wataangazia masuala ya uchumi wa eneo la Magharibi.

“Tumepata kibali kipya kuandaa mkutano uwanjani Nabongo mnamo Januari 25. Tutaangazia masuala ya uchumi na jinsi tunavyoweza kunusuru viwanda vya eneo la Magharibi,” akasema Bw Echesa.