Habari

Matiang'i apewa mamlaka zaidi ya kudhibiti mikutano ya kisiasa

October 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i sasa ndiye atasimamia kamati maalum itakayodhibiti mikutano ya hadhara kuzuia kutokea kwa visa vya utovu wa amani nchini.

Hii ni baada ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi kuidhinisha kuundwa kwa kamati hiyo itakayoshirikisha wawakilishi kutoka wizara mbalimbali na itakayosimamia utekelezaji wa masharti kali kuhusu mikutano ya hadhara.

Kamati hiyo itashirikisha wawakilishi kutoka Wizara za Usalama, Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Teknolojia ya Habari ya Mawasiliano (ICT), Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA).

“Wajibu wa kamati hiyo maalimu ni kufuatilia, kunakili na kuhakikisha utekelezaji wa masharti kuhusu maandalizi ya mikutano ya hadhara na maandamano,” ikasema taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo wa baraza la mawaziri.

Ikaongeza: “Kamati hiyo pia itafuatilia upeperushaji, uchapishaji na usambazaji wa habari na kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhakikisha kuwa hayachochei chuki, uhasama wa kikabila, na kuvuruga amani na uthabiti nchini.”

Kimsingi, Baraza la Mawaziri liliidhinisha masharti yote ya kudhibiti mikutano ya hadhara yaliyotolewa Jumatano na Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) chini ya uongozi wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.

Kulingana na masharti hayo, wanasiasa wanaotaka kufanya mikutano ya kisiasa wanafaa kupata idhini kutoka Mkuu wa Polisi kutoka eneo hilo siku tatu kabla.

Vile vile, waandalizi wa mikutano kama hiyo wanafaa kushirikiana na maafisa wa polisi kudumisha usalama katika mikutano kama hiyo.

Aidha, chini ya masharti hayo, waandalizi wa mikutano hiyo watawajibikia fujo zozote ambazo huenda zitakatoa.

Navyo, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimeonywa dhidi ya kupeperusha matamshi ya chuki yanatolewa na wanasiasa katika makujwaa yao.

Vyombo vya habari ambavyo vitapatikana na hatia ya kukiuka kanuni hiyo vitaadhibiwa kwa kutozwa faini isiyozidi Sh1 milioni.

Naibu Rais William Ruto alihudhuria kikao cha baraza la mawaziri ambapo masharti hayo ya kamati ya NSAC yaliidhinishwa.

Hayo yakijiri, maafisa waliwatawanya raia na waandalizi wa mkutano wa hadhara ambao Dkt Ruto alikuwa ameratibiwa kuhutubia katika uwanja wa shule ya upili ya Kebirigo, kaunti ya Nyamira.

Baada ya vuta nikuvute ya saa kadha kati ya polisi, wabunge na waandalizi wa mkutano huo ambao ulikuwa wa kuchanga fedha za kusaidia makundi ya waendesha bodaboda.

Naibu Rais alitangaza kuahirishwa kwa mkutano huo hadi Alhamisi wiki ijayo.