Matiang’i apotosha kuhusu uhalifu

Matiang’i apotosha kuhusu uhalifu

Na WANDISHI WETU

WATU kadhaa nchini wanauguza majeraha waliyopata mkesha wa Krisimasi licha ya Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i kusisitiza kuwa kudai hakukuwa na visa vyovyote vya uhalifu vilivyoripotiwa kote nchini kipindi hicho.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umegundua kuwa wahalifu hawakwenda mapumzikoni, na badala yake waliendelea kuhangaisha Wakenya kwa kutekeleza mauaji, wizi wa mabavu na maovu mengineyo.

Dkt Matiang’i na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, awali walikuwa wamehakikishia Wakenya kuwa usalama ungeimarishwa kote nchini.

Bw Mutyambai hata aliagiza maafisa wa usalama waliokuwa likizoni kurejea kazini ili kulinda Wakenya wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

“Hatujapokea ripoti yoyote kuhusu kisa cha uhalifu. Hali ya utulivu imetanda kote nchini isipokuwa changamoto chache zinazohusiana na usafiri,” akasema Dkt Matiang’i.

Lakini taarifa zilizoandikishwa katika vituo vya polisi zinaonyesha kuwa kulikuwa na shughuli tele za uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini.Wahalifu waliendelea kutekeleza maovu hata baada ya sherehe za Krismasi.

Jumatatu, Mahakama ya Makadara ya jijini Nairobi ilikuwa na kesi tele zinazohusiana na washukiwa waliokamatwa kati ya Desemba 24 na Desemba 27.Mfano, Desemba 24, katika eneo la Lugari, mwili wa Edward Kibwasi ulipatikana karibu na baa maarufu inayojulikana kama Life Bar.

Mwili huo ulikuwa na majeraha usoni na kwenye mikono. Damu ilikuwa ikivuja kutoka mdomoni.Maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kiini cha kifo cha Kibwasi.

Gazeti la Taifa Leo pia lilifanikiwa kuona ripoti kuhusu visa vingine 10 ambapo watu waliuawa mkesha wa Krismasi.Pia kulikuwa na visa vingi vya fujo manyumbani.

Katika eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, mwanaume alijinyonga baada ya kumjeruhi vibaya mkewe kwenye mzozo wa kinyumbani

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Polisi wakomeshe dhuluma kwa raia

Maraga kustaafu baada ya pandashuka tele akiongoza mahakama