Matiang’i apumua baada ya msamaha

Matiang’i apumua baada ya msamaha

NA WAANDISHI WETU

HATUA ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kutupilia mbali ‘mashtaka’ dhidi ya aliyekuwa waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i imeanika serikali ya Kenya Kwanza iliyokuwa imeahidi kutotumia polisi kuhangaisha viongozi wa upinzani.

Bw Haji jana Jumatatu aliagiza mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin kutamatisha uchunguzi dhidi ya Dkt Matiang’i kuhusu madai kwamba polisi walivamia makazi yake mtaani Karen mnamo Februari 9, 2023.

Kupitia taarifa iliyotiwa saini na naibu DPP, Lilian Obuo, Bw Haji alisema “hakuna ushahidi wa kutosha kumfungulia Dkt Matiang’i na (wakili Danstan) Omari mashtaka ya kutoa habari za kupotosha kwa umma na matumizi mabaya ya mitandao”.

“Baada ya kutathmini kwa kina ushahidi uliowasilishwa pamoja na taarifa za mashahidi, DPP amebaini hakuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki Dkt Matiang’i na wakili Omari,” nakala ya taarifa kutoka kwa DPP iliyotiwa saini na Bi Obuo ilisema.

Amri kuwa DCI akome mara moja kumchunguza Dkt Matiang’i inaonekana kuashiria maafikiano kati ya waziri huyo wa zamani wa usalama na serikali. Vilevile, inatoa dalili kuwa yamkini polisi walivamia nyumbani kwa Dkt Matiang’i kwa sababu za kisiasa na wala si uhalifu.

Mara nyingi, DPP hushauri maafisa wa DCI kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ushahidi thabiti. Lakini kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo ni ishara kwamba polisi walishindwa kujiondolea madai kwamba walivamia makazi ya Dkt Matiang’i.

Alhamisi, kundi la wabunge wa Azimio la Umoja, kutoka Kisii walikutana na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi na kumuomba amsamehe Dkt Matiang’i.

Katika mkutano huo, duru zilieleza Taifa Leo, Rais Ruto alishikilia kuwa hakuwaagiza maafisa wa polisi kumwandama Dkt Matiang’i. Rais alilaumu Dkt Matiang’i kwa kujiletea masaibu kwa kudai kwamba polisi walivamia nyumbani kwake.

Duru zinaarifu Jumapili, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alikutana na Dkt Matiang’i pamoja na viongozi mbalimbali kutoka eneo la Gusii katika juhudi za kumuokoa waziri huyo wa zamani.

Mkutano huo wa Bw Machogu na Dkt Matiang’i ulifanyika katika Kituo cha Hisabati na Sayansi Afrika (CEMASTEA), taasisi ya umma iliyoko mtaani Karen, Nairobi.

Wengine waliokuwepo katika mkutano huo ni Wakili wa Serikali Mteule Shadrack Mose, mbunge wa Mugirango Kaskazini na mwenyekiti wa wabunge wa Gusii Joash Nyamoko, na wabunge wa zamani Jimmy Angwenyi na Zebedeo Opore, viongozi wa Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) John Simba na Steve Omenge.

Bw Omenge ndiye mlezi wa kundi la wasomi kutoka Gusii na aliwahi kuwa meneja wa kampeni za chama cha Jubilee.

Ilibainika kuwa Bw Machogu amekuwa akiongoza juhudi za kuwapatanisha Rais Ruto na Dkt Matiang’i.

Mkutano wa Jumapili ulijumuisha wabunge wa sasa na zamani pamoja na viongozi wa kidini. Juhudi hizo za kupatanisha Rais Ruto na Dkt Matiang’i zinajiri huku Kiongozi wa Nchi akijiandaa kuzuru Kisii katika hafla ya kumkaribisha rasmi nyumbani Bw Machogu hapo Machi 24.

Kuhangaishwa kwa Dkt Matiang’i hivi majuzi kumepandisha joto la kisiasa katika Kaunti za Kisii na Nyamira.

“Ni kweli, tulikutana. Bw Machogu na Dkt Matiang’i walikuwepo. Tunachotaka ni kuunganisha watu wetu na jamii nzima. Tulisikiliza Dkt Matiang’i naye akatusikiliza pia. Mkutano ulizaa matunda,” Bw Nyamoko akaambia Taifa Leo.

Duru zinasema kuwa mkutano huo ulikuwa na “baraka za Rais Ruto”.

“Hatuwezi kuendelea kupigana sisi kama jamii. Jamii nyingine zimeungana na zimekuwa zikilinda watu wao. Wakati wa kuungana ni sasa ili tuzungumze kwa sauti moja,” akasema Bw Nyamoko.

“Matiang’i huenda alikosea wengi alipokuwa waziri. Aliomba msamaha. Inaonekana kauli yake aliyotoa wakati wa mazishi ya aliyekuwa waziri wa Elimu George Magoha huenda ilikera viongozi serikalini.”

Kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, mwaka jana, mrengo wa Kenya Kwanza ulishutumu Dkt Matiang’i kwa kutumia polisi kutesa na kuhangaisha wandani wa Dkt Ruto.

Viongozi wa Kenya Kwanza aliapa kutenga polisi na masuala ya siasa baada ya kuingia mamlakani.

  • Tags

You can share this post!

Wazee zaidi ya 100 wapata matibabu ya bure kupitia mpango...

Gaspo Women wako ngangari kutwaa ubingwa, watuma salamu kwa...

T L