Matiang’i apuuza kilio cha Naibu Rais

Matiang’i apuuza kilio cha Naibu Rais

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i amepuuzilia madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba polisi wamefeli kukomesha ghasia ambazo zimekumba baadhi ya mikutano yake ya kampeni.

Dkt Matiang’i jana Jumatatu alisema fujo hizo husababishwa na tofauti baina ya makundi ya watu ambao hung’ang’ania pesa ambazo Dkt Ruto huwapa ili wamuunge mkono.

“Inasikitisha kuwa yule aliandika barua hiyo kwamba hapewi ulinzi wakati anafanya mikutano yake ya kisiasa hulindwa na zaidi ya maafisa 50 wa polisi katika mikutano. Fujo anazorejelea na yeye mwenyewe huchochea kupitia pesa anazowapa vijana pamoja na ahadi nyingine asizoweza kutimiza,” Dkt Matiang’i akasema.

“Isitoshe, yule ambaye aliandika barua hiyo anaketi katika Baraza la Kitaifa la Usalama. Hii ni kinaya kwa sababu hapo ndipo masuala ya usalama hujadiliwa,” akaongeza.

Dkt Matiang’i alisema hayo kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi baada ya kuongoza mkutano wa wa asasi za usalama kujadili mikakati ya kudumisha usalama nchini wakati huu wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Aliandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti miongoni mwa wengine.

Dkt Matiang’i alikuwa akirejelea barua ambayo chama cha United Democratic Alliance (UDA) kilimwandikia Rais Uhuru Kenyatta kikilalamikia kisa ambapo fujo zilitokea katika mkutano wa Dkt Ruto katika eneo bunge la Embakasi Mashariki.

Katika barua hiyo ambayo nakala yake ilitumiwa Dkt Matiang’I na kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kitaifa ya uhalifu (ICC), chama hicho kilidai kuwa fugo zilisababishwa na wafuasi wa ODM, “wakisaidiwa na polisi”.

Bw Matiang’i aliwaambia wanasiasa kuendesha kampeni zao kwa amani na wakome kutoa matamshi ambayo yanaweza kuchochea chuki na uhasama wa kisiasa na kikabila.

“Vile vile nawaonya wanasiasa dhidi ya kuwasuta maafisa wa usalama kwa maneno wanapotekeleza majukumu yao kwa sababu hawana jukwaa la kujitete,” akasema.

Dkt Matiang’i aliwataka maafisa wa usalama kufanya kazi yao bila woga wala mapendeleo yoyote haswa wakati huu wa kampeni za kisasa.

“Nataka kusisitiza tena kwamba msiruhusu vitisho vya kisiasa kuyumbisha utekelezaji majumu yenu kulingana na kiapo chenu. Mwapaswa kutekeleza kazi zenu bila uwoga wala mapendeleo na msisikilize vitisho kutoka mtu yeyote hata kama ni wanasiasa,” Dkt Matiang’i aliwaambia maafisa wa polisi.

Waziri alisema tangu mwanzoni mwa mwaka huu kumetoa visa vinne pekee vya ghasia zinazohusiana na siasa ambazo maafisa wa polisi wameshughulikia kikamilifu.

“Kwa mfano, katika kisa cha Busia, washukiwa wamefikishwa mahakama ili sheria ifuate mkondo wake,” Dkt Matiang’i akasema.

Hata hivyo, Waziri alisema hali ya usalama nchini ni shwari na kwamba hakujaripotiwa visa ambapo “watu fulani wanapanga kutekeleza uhalifu kwa sababu zozote zile zikiwemo za kisiasa.”

Lakini Dkt Matiang’i aliwashauri wananchini kuendelea kuchukua tahadhari haswa kuhusiana na visa vya mashambulio ya kigaidi yalishuhudiwa katika kaunti ya Lamu na maeneo mengine ya Pwani ya Kenya.

You can share this post!

Vijana wazindua kampeni ya kutoa uhamasisho wa uandikishaji...

ALI SHISIA: Kiswahili kama chombo cha umoja na maendeleo...

T L