Habari Mseto

Matiang’i asisitiza kuwakabili vilivyo wale anaowaita 'wachochezi'

October 11th, 2020 1 min read

Na RUTH MBULA

WAZIRI wa Usalama Fred Matiang’i amewataka Wakenya wawakatae watu ambao matamshi yao yanaweza kuingiza nchi kwenye machafuko.

Aliionya jamii ya Abagusii ijichunge sana dhidi ya watu fulani anaodai walichochea fujo katika sehemu za nchi, zilizosababisha maelfu ya watu kupoteza makao.

“Watu hao walichochea jamii nyingine dhidi ya jamii ya Abagusii na sasa wanajaribu kujifanya marafiki wakiomba kura, ingawa Uchaguzi Mkuu uko miaka miwili ijayo,” akasema Dkt Matiang’i.

Alionya kwamba siasa za chuki zinazoshuhudiwa wakati huu ni hatari kwa nchi. Aliapa kwamba serikali itawakabili vilivyo watu hao, bila kujali nafasi zao katika siasa au jamii.

Dkt Matiang’i alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Nyamira wakati wa shehere ya kutoa shukrani katika makanisa ya Makairo na Omwobi SDA.

“Hatutaki wanasiasa wanaojinufaisha na siasa za kugawanya watu. Hatuzitaki siasa hizi za kuwagawa Wakenya katika makundi kwa jina la kutaka kushinda uchaguzi,” akasema.

Alieleza kwamba urais ni ishara ya umoja na anayekalia kiti kwenye afisi hiyo ni lazima apewe muda wa kutosha kutekeleza majukumu aliyopewa na Katiba, bila ya kutatizwa kama inavyoshuhudiwa.

Dkt Matiang’i alilalama kuwa baadhi ya vijana wameanza kuhadaiwa na wanasiasa wanaoendeleza siasa za chuki, na kuwafanya kuwa maajenti wa uvunjaji sheria.

Aliwaonya vijana hao pamoja na wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya, kwamba chuma chao ki motoni.

“Ni lazima tuwafunze vijana wetu kuwa waaminifu, kuheshimu na kuwajibika. Lazima tuwafunze kuwa wakweli na waelewe maadili yetu. Hatutakubali wahadaiwe na kuacha njia hiyo,” akasema.