Habari

Matiang'i atakiwa kueleza sababu ya makarani wa Huduma Namba kutolipwa

November 26th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamemtaka Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani Fred Matiang’i na Katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho kufika mbele yao Jumatano kueleza ni kwa nini malipo ya walioendesha shughuli ya usajili wa Huduma Namba yamecheleweshwa.

Kulingana na wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Usalama wa Kitaifa, Ulinzi na Mahusiano ya Kimataifa, zaidi ya miezi sita imepita baada ya kukamilishwa kwa shughuli hiyo ilhali makarani walioendesha kazi hiyo hawajalipwa.

“Tunataka waziri Matiang’i kufika mbele ya kamati yangu kueleza ni kwa nini makarani hao hawajalipwa ilhali mpango wa Huduma Namba ulitengewa Sh8.5 bilioni kutoka Wizara ya Fedha,” mwenyekiti wa Kamati hiyo Yusuf Haji akasema.

Kamati hiyo pia inataka waziri Matiang’i na Katibu wake Dkt Kibicho kueleza ni kwa nini zaidi ya Wakenya 37 milioni ambao walisajiliwa kwa Huduma Namba hawajapewa kadi zao hadi wakati huu.

“Baada ya Sh8.5 bilioni kutumika kuchukua maelezo ya Wakenya kidijitali, tunashangaa kwamba miezi sita baadaye hawajapewa kadi hizo. Tunataka kuelezwa ni lini kadi hizo zitatolewa kwa Wakenya,” akasema Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior.

Wasiwasi

Seneta huyo alisema kuwa Wakenya wameingiwa na wasiwasi kwamba huenda walihadaiwa na maelezo yao yakachukuliwa mwa malengo ‘fiche’.

“Kuna wasiwasi miongoni mwa Wakenya. Tunafahamu kwamba katika jamii yenye ustaarabu, thamani ya pesa zao ni muhimu. Kwa hivyo, wanataka kujua thamani ya pesa zilizotumiwa katika usajili wa Huduma Namba kwa kupewa kadi zenyewe ili waweze kuzitumia,” Bw Kilonzo Junior akaeleza. Kauli yake iliungwa mkono na Seneta wa Migori Ochillo Ayacko.

Seneta wa Kitui Enock Wambua alitaka Bw Matiang’i kueleza ni kwa nini wizara yake juzi iliomba itengewe Sh1 bilioni zaidi, katika bajeti ya ziada, za kuchapisha kadi za Huduma Namba.