Na WYCLIFFE NYABERI
WAZIRI wa Usalama wa Kitaifa, Fred Matiang’i jana Ijumaa aliashiria kuwa Rais Uhuru Kenyatta anaunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Bw Odinga jana Ijumaa alijawa na furaha baada ya Dkt Matiang’i kutangaza kuwa atamuunga mkono kwenye azma yake ya kuingia Ikulu mwaka 2022.
Dkt Matiang’i alisema yeye anafuata maelekezo ya Rais Kenyatta na “siwezi kuunga mkono mtu ambaye Rais hataki.”
Hafla iliyolenga kuchangisha pesa za kusaidia ujenzi wa shule kutwa ya upili ya Mwongori, inayopatikana Borabu kwenye kaunti ya Nyamira, ilitumiwa kama jukwaa la Dkt Matiang’i kutangaza mwelekeo ambao angependa jamii yake ifuate katika siasa za 2022.
Katika siku za hivi punde, baadhi ya wabunge wa jamii ya Abagusii wamekuwa wakimwuliza waziri Matiang’i awape mwelekeo watakaofuata kisiasa.
Bw Odinga alilengalengwa na machozi ya furaha baada ya umati mkubwa uliokuwapo shuleni humo kumhakikishia kuwa utamuunga mkono kupitia kwa waziri huyo.
Hatua hiyo ilimgusa sana moyoni Bw Odinga aliyesema amejihisi mwepesi na mchache wa maneno.
“Sitaki niendelee hata zaidi kwani yale Fred amesema yamenigusa sana. Kwa kweli sikutarajia haya. Namshukuru na nitatembea naye,” Bw Odinga akasema.
Kinara huyo alidokeza yeye na Dkt Matiang’i walikuwa wamejadiliana na kuelewana kwamba Bw Odinga awanie kiti hicho.
“Tulishauruana na kukubaliana niwe mtu wa kwanza kukabiliana na fisi msituni,” Bw Odinga akaeleza umati ulioshangilia.
Kwa mara ya kwanza, Dkt Matiang’i alimshambulia hadharani naibu Rais William Ruto akisema amekuwa akilalamika kutengwa serikalini ilhali wakati mwingine anajivunia ufanisi wa miradi ya serikali.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema tangu taifa la Kenya lijinyakulie uhuru, maeneo ya Mlima Kenya na Nyanza yamekuwa yakitembea pamoja.
Mwenzake wa ulinzi Eugene Wamalwa aliomba Wakenya waweke amani uchaguzi mkuu unapokaribia.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni magavana James Ongwae (Kisii), Amos Nyaribo (Nyamira), Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini), Junet Mohammed na Jimmy Angwenyi miongoni mwa wengine.