Habari

Matiang'i atangaza vita dhidi ya mihadarati

August 12th, 2019 1 min read

MOHAMMED AHMED NA MISHI GONGO

WAZIRI wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i ameanzisha upya vita dhidi ya dawa za kulevya katika Pwani ya Kenya, akitaja dawa hizo kama sababu kuu ya vijana kujiunga na magenge ya ujambazi.

Dkt Matiangi alisema vita hivyo vitakuwa vikali licha ya hatari inayohusishwa na biashara haramu ya mihadarati.

Akizungumza katika mkutano uliohusisha maafisa wa usalama na wanasiasa wa Mombasa, Dkt Matiang’i alisema amejitayarisha kukabiliana na janga hilo yeye binafsi.

“Tumejitayarisha katika vita hivi na hatutalegeza kamba hadi pale tutakapohakikisha wahusika wote wamehukumiwa,” akasema

Wanasiasa waliohudhuria waliongozwa na Naibu Gavana wa Mombasa William Kingi, Seneta Mohammed Faki na wabunge Abdulswamad Nassir (Mvita), Mohammed Ali (Nyali) na Mishi Mboko (Likoni).

Dkt Matiang’I, ambaye aliandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai, alisema kuna uhusiano kati ya ulanguzi na usambazaji wa dawa za kulevya, wanasiasa, matajiri na magenge ya ujambazi.

Alieleza kuwa suala la madawa ya kulevya Pwani kwa jumla limekuwa mwiba kwa serikali, hivyo imewabidi kuanzisha mbinu mpya za kukabiliana nao ikiwemo kuchunguza polisi na watumishi wa serikali.

“Hakuna atakayeachwa nje katika vita hivi. Tumeanzisha mikakati ya kupiga darubini kitengo cha usalama na wengineo,”alisema.

“Hatuwezi kusalimisha nchi yetu kwa majambazi. Maafisa wa usalama watapelekwa sehemu zilizo na visa vya ujambazi sugu ili kupambana navyo,” alisema.

Bw Kingi alisema viongozi wataungana na maafisa wa usalama kufanikisha operesheni dhidi ya walanguzi na magenge.

Waziri Matiang’i alifanya ziara yake kufuatia tukio la mashabulio wiki iliyopita katika eneo la Bamburi, ambapo watu 13 walijeruhiwa.

Duru zilisema tukio hilo lilisababishwa na kutofautiana kwa walanguzi wawili wa madawa ya kulevya baada ya shughuli zao kuingiliana.

Habari zilisema mmoja wa walanguzi hao aliamua kukodi magenge kuvamia mwenzake na washirika wake, kisha kuvamia na kupora wafanyibiashara Bamburi baada ya shambulio.