Siasa

Matiang’i atosha 2022, Murathe asema

February 29th, 2020 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

ALIYEKUWA naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe amemsifu Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi akisema ndiye anayefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Murathe aliwaongoza wanasiasa wa eneo la Mlima Kenya na Kisii kummiminia sifa Bw Matiang’i kwa kumuunga mkono Rais Kenyatta na wakasema anatosha kuwa Rais.

Akiongea katika uwanja wa michezo wa Gakoigo wakati wa sherehe ya shukrani ya kamishna wa Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Wambui Nyutu, Bw Murathe ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta alisema Matiangi ndiye anayestahili kuwa Rais kwa sababu ameonyesha uwazi na ukakamavu katika uongozi.

“Nchi hii inahitaji kiongozi kama Bw Matiang’i; ni mwaminifu na hana doa katika maadili yake na ninataka kukariri yale ambayo nimekuwa nikisema, kwamba Rais wetu hatamwachia mamlaka mtu mwizi. Tuendelee kumuunga Dkt Matiangi anyoroshe nchi kwa manufaa ya Wakenya,” Bw Murathe alisema.

Mbunge wa Kitutu Chache Richard Onyonka alitaka kuwe na ushirikiano wa jamii za Wakikuyu na Wakisii kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 akisema zinaweza kutoa rais.

“Jamii yetu imetoa mwana ambaye amethibitisha kwamba anaweza kuwa kiongozi shupavu na ameaminiwa na rais, sasa ameiva kuongoza nchi na ni ningetaka jamii za Wakisii na Wakikuyu zikiungana kumuunga mkono,” alisema Bw Onyoka.

Hata hivyo, Dkt Matiang’i aliposimama kuhutubu alisema jukumu lake ni kutekeleza ajenda za Rais Kenyatta na akawataka wanasiasa waache afanye kazi yake.

“Ninawataka viongozi waache tufanye kazi ambayo tumepatiwa na Rais, tumejitolea kuhakikisha serikali ya Jubilee itatimiza ahadi ilizowapa Wakenya” alisema.

Bw Matiangi alipuuza miito ya wanasiasa hao na kusisitiza anatelekeza maagizo ya Rais Kenyatta.