Habari Mseto

Matiangi azima 'Disco Matanga' Kilifi kupunguza mimba za mapema

January 8th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi amepiga marufuku hafla za matanga ya kuomboleza wafu ambazo zinazopita saa tano usiku katika Kaunti ya Kilifi, kama mbinu ya kuimarisha usalama.

Dkt Matiangi Jumatatu alisema kuwa hafla hizo zinazojulikana kama Disco Matanga zimekuwa zikitoa nafasi kwa wahalifu kuendesha shughuli zao.

Alisema kuwa japo hafla hizo zimekuwa zikichukuliwa kuwa namna ya kuhifadhi utamaduni na jamii nyingi, kuongezeka kwa kiwango cha uhalifu eneo hilo sasa kunazua hofu.

“Hiki kitu kinachoitwa Disco Matanga si njia ya utamaduni tena. Wahalifu wanatumia fursa hiyo kuendesha vitendo vyao,” akasema waziri huyo.

Dkt Matiangi alizungumza wakati alipomtembelea chifu David Kahindi ambaye alivamiwa alipokuwa akijaribu kuzuia moja ya hafla hizo eneo la Shariani, kaunti ya Kilifi.

Bw Kahindi amelazwa katika hospitali ya Jocham, Mombasa kufuatia majeraha aliyopata wakati huo alipovamiwa.

Dkt Matiangi alisema kuwa serikali ina rekodi zinazoonyesha kuwa dawa za kulevya zinasambazwa na kuuzwa katika hafla hizo, mbali na wasichana kunajisiwa.

“Visa vya mimba za mapema Kilifi vimehusishwa na huu upuuzi unaoitwa Disco Matanga. Tumeelewana leo na nimefahamisha kamishna wa kaunti ya Kilifi na timu yake ya walinda usalama kuwa hafla hizo sharti ziishe kufikia saa tano usiku,” akasema.

Alisema yeyote atakayepatikana akiendesha hafla hizo baada ya hizo saa atakamatwa na kufikishwa kortini.