Habari Mseto

Matiang'i lawamani kukosa kuzuru eneo la mauaji

March 10th, 2019 1 min read

Na DERICK LUVEGA

WABUNGE watatu wamemkosoa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kwa kukosa kutembelea soko la Kilingili kufuatia mauaji ya askari gongo sita Jumapili iliyopita.

Wabunge hao ambao ni Alfred Agoi (Sabatia), Ben Shinali (Ikolomani) na Omboko Milemba (Emuhaya) walimpa waziri huyo makataa ya hadi Ijumaa kutembelea soko hilo lililo kwenye mpaka wa Kaunti za Vihiga na Kakamega.

Walisema akikosa kufanya hivyo itakuwa ni heri ajiuzulu kutoka kwa wadhifa wake.

Wabunge hao walioongozwa na Bw Milemba walikuwa wanahutubia wakazi wenye ghadhabu katika soko hilo Jumamosi jioni baada ya kutembelea familia zilizoathirika na wakakutana na polisi katika kituo kilicho mita 50 pekee kutoka kwa soko hilo.

“Wakati wewe (Matiang’i) ulipohudumu kama Waziri wa Elimu, ulikuwa ukienda shuleni haraka sana wakati wowote kulipotokea shida. Ukikosa kuja eneo hili ifikapo Ijumaa, inafaa ujiuzulu,” akasema Bw Milemba.

Alisema wanataka Dkt Matiang’i akague hali ya usalama eneo hilo kibinafsi “ndipo atambue jinsi maafisa wake walivyolegea kazini.”

“Mbona Matiang’i hajazuru mahali hapa baada ya kisa hicho cha kinyama? Nguvu alizokuwa akionyesha katika sekta ya elimu ndizo zilimfanya aajiriwe kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani,” akasema Bw Milemba.

Hisia zake ziliungwa mkono na Bw Shinali ambaye alisema suala hilo litapelekwa bungeni endapo waziri atakaidi wito wao.

Bw Shinali pia alikosoa sera inayohitaji polisi kuishi nje ya vituo vyao na kusema hali hiyo itawafanya kuzembea katika upigaji doria.