Habari MsetoSiasa

Matiang'i na Mutyambai waitwa Seneti kueleza sababu ya kuhangaisha maseneta

August 18th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Seneti Kenneth Lusaka Jumanne aliamuru Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai wafike mbele ya seneti kuelezea kiini cha kukamatwa kwa maseneta watatu Jumatatu asubuhi.

Maseneta Cleophas Malala (Kakamega), Christophet Lang’at (Bomet) na Stephen Lelengwe (Samburu) walikamatwa na maafisa kitengo cha upelelezi wa jinai (DCI) walipokuwa wakijiandaa kuhudhuria kikao cha seneti kujadili mfumo wa ugavi wa fedha.

Maafisa wa usalama walizingira makazi ya Bw Malala na Dkt Lang’at walidai walitumwa na “wakubwa wetu” kuwakamata ilhali Bw Lelengwe alikamatwa eneo la River Side akielekea majengo ya bunge.

Bw Lusaka aliwataka Dkt Matiang’i na Bw Mutyambai kufika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Usalama kutoa ufafanuzi kuhusu sababu zilizopelekea maseneta hao kukamatwa.

“Bunge hili lingependa kufahamishwa ikiwa kukamatwa kwa watatu hao kuna uhusiano wowote na wajukumu hao kama maseneta na haswa suala hili la mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti,” akasema.

Hata hivyo, awali,  Seneta Malala aliwaambia wanahabari nyumbani kwake eneo la Kitengela kwamba alifahamishwa kuwa maafisa wa polisi walitumwa wamkamate kwa kugawanya sanitiza mjini Mumias Jumapili.

Ilidaiwa kuwa Seneta Malala aliendesha shughuli hiyo bila kuzingatia masharti ya Wizara ya Afya ya kudhibiti Covid-19 kuwa kutowakusanya watu wengi mahala pamoja.

“Ukweli ni kwamba hizi ni njama za kunitisha na kunizuia kufika bungeni kutekeleza wajibu wangu kama seneta wa Kakamega kwa kupinga mfumo wa ugavi wa fedha utakaligawanya taifa hili,” akasema.

Naye Seneta wa Turkana  Profesa Malachi Ekai alisema Seneta Lelengwe alikamatwa kuhusiana na kisa cha wizi wa mifugo katika kaunti ya Samburu.

Naye  wakili wa Dkt Langat Nelson Havi alisema mteja wake alikamatwa kwa madai kuwa aliwalisha kiapo vijana 200 ili wawashambulie watu wa jamii ya Wamaasai.

Hata hivyo, Mbw Lelengwe na Lang’at waliachiliwa huru Jumatatu jioni baada ya kufikishwa Samburu na Bomet, mtawalia, huku Malala akiachiliwa Jumanne.