Habari Mseto

Matibabu ya bure yawafaa wakazi wa Nakuru wenye matatizo ya macho

June 2nd, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Hospitali ya Rufaa ya Nakuru wiki hii imeandaa warsha ya kuwapa wagonjwa wenye matatizo ya macho tiba bila malipo, huku shughuli yenyewe ikitamatika Jumapili.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Daktari Joseph Njihia, mtaalamu wa macho anasema serikali ya Kaunti ya Nakuru ilishirikiana na AMRITA Kenya, shirika la kibinafsi linalowasaidia watu wasiojiweza katika jamii.

Alieleza kuwa wenye matatizo ya macho wanaendelea kupata upasuaji wa bure,zaidi wakilenga wazee walio katika hatari ya kupofuka.

“Kufikia mwisho wa zoezi hili tunatarajia kufanya upasuaji kwa wagonjwa baina ya 250-300,ambapo tayari watu 110 wamehudumiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani,” Njihia akasema.

.Maafisa wa afya wa kujitolea kutoka humu nchini na nchi za ugenini waliojitolea kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya macho katika hospitali ya rufaa ya Nakuru PGH. Picha/ Richard Maosi

Zoezi zima linawaleta pamoja madaktari 10 wa kujitolea kutoka taifa la Uhispania, na wengine 30 kutoka Kenya.

Robert Njoroge mkaazi wa Nakuru anasema alipata habari kuhusu matibabu haya tangu wiki mbili zilizopita,na akapatiwa mwaliko wa kutembelea PGH tarehe 29 mwezi huu.

Anasema matatizo ya macho yalimfanya ashindwe kuendesha gari kwa sababu hakuwa akiona vizuri na hali hiyo ilifanya azivunje sheria nyingi za barabarani bila kupenda..

Aliamua kutembelea hospitali ili afanyiwe uchunguzi wa kina, na akapata afueni alipoelezwa kuwa upasuaji ungempatia nafasi ya kupata tiba ya kudumu.

“Ni kama Mungu amejibu maombi yangu kwa sababu kuanzia sasa, nitakuwa na uwezo wa kuona vyema,” alisema Bw Njoroge akielekea kwenye chumba cha kufanyia upasuaji.

Aidha Daktari Isabel Signes kutoka Uhispania anasema kaunti ya Nakuru imebahatika kupata madaktari wa kigeni, watakaoshirikiana na wale wa humu nchini kuwasaidia wagonjwa watu wenaougua macho..

Alieleza kuwa jukwaa hili litawaongezea matabibu wa humu nchini ujuzi na kuboresha taaluma zao kuanzia utafiti hadi kwenye matibabu.

Kulingana naye watu wengi nchini wana matatizo ya macho ila hawana uwezo wa kumudu matibabu ambayo ni bei ghali. Picha/ Richard Maosi

Anaona ni vyema endapo serikali itapunguza gharama ya kutoa matibabu kwa walio na matatizo ya macho kwani kulingana naye wengi wao ni wazee.

“Wengi walio na matatizo ya macho tumebaini wanaugua maradhi ya sukari au shinikizo la damu ambapo kiwango cha sukari mwilini pia huadhiri uwezo wa macho kuona,” alisema.

Wagonjwa waliopata huduma ya bure ya macho wanatokea mbali na karibu ya kaunti ya Nakuru.

Mmoja wao ni Esther Wambui kutoka Mau Narok.Akiwa na miaka 68 anasema amekuwa na tatizo la Macho takriban miaka 10 iliyopita.

Alianza kujikuna macho kisha yakabadili rangi na kuwa mekundu,anasema mbali na kutafuta matibabu kwenye hospitali kadhaa za kibinafsi amekuwa akipokea tembe za kumeza.