Habari Mseto

'Matibabu ya nyumbani yamesaidia watu 2,738 kupona'

July 22nd, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU
Wakenya wamehimizwa kukumbatia mpango wa matunzo na matibabu nyumbani kwa watu wanaopatikana na ugonjwa wa Covid-19. 
Wizara ya Afya imesema gharama ya mpango huo ni nafuu, ikilinganishwa na matunzo hospitalini.
Waziri Msaidizi katika Wizara Dkt Rashid Aman Jumatano alisema mpango huo umeonekana kufaulu.
Alitangaza kwamba jumla ya wagonjwa 2,738 wanaotunzwa na kutibitiwa nyumbani wamethibitishwa kupona kufikia sasa.
Tangu Kenya itangaze kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona mnamo Machi 13, 2020, jumla ya wagonjwa 6,757 wamethibitishwa kupona kabisa.
“Mpango wa nyumbani si ghali ukilinganishwa na matunzo na matibabu ya hospitali. Asilimia 90 ya wagonjwa hawaonyeshi dalili, idadi ambayo inaweza kuhudumiwa nyumbani. Hii inaonyesha tunaweza kukabiliana na asilimia 10 ya wanaonyesha dalili za Covid-19 katika vituo vya afya,” akasema Dkt Aman.
Akipigia upatu mpango huo ulioanzishwa miezi miwili iliyopita, Waziri alisema utasaidia kupunguza msongamano katika vituo mbalimbali vya afya nchini, vinavyotoa matunzo ya corona.
Mgonjwa anayetunziwa nyumbani lazima awe na cheti cha Wizara ya Afya, kuashiria kwamba haonyeshi dalili zozote za corona licha ya kuthibitishwa kuambukizwa virusi.
Wizara pia inasisitiza anakotunziwa, sharti kuwe na nafasi ya kutosha ambapo anapaswa kuwa na choo na bafu yake pekee.
Wakati huohuo, Wizara ya Afya Jumatano ilitangaza maambukizi mapya 637 yaliyothibitishwa kutoka kwa sampuli 4,275 zilizofanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Takwimu hiyo inafikisha jumla ya visa 14,805 vya Covid-19 nchini.
Kufikia sasa, jumla ya sampuli 254,273 zimefanyiwa vipimo.
Katika maambukizi mapya ya Jumatano, 623 ni Wakenya na 14 wakiwa raia wa kigeni. “Mkondo wa wanaume kuwa waathiriwa wakuu unaendelea kushuhudiwa ambapo katika visa vya leo, wameandikisha 361 nao wanawake wakiwa 276. Mgonjwa wa umri mdogo amekuwa na mwaka mmoja na yule mkubwa miaka 88,” akaeleza Waziri Aman.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wagonjwa 499 walithibitishwa kupona, kati ya idadi hiyo 406 wakiwa wanaotunziwa nyumbani na 93 kutoka vituo mbalimbali vya afya nchini. Idadi jumla ya waliopona nchini imefika 6,757.
Wizara pia ilitangaza wagonjwa 10 kufariki, takwimu hiyo ikifikisha jumla ya watu 260 walioangamizwa na Covid-19 nchini.