Kimataifa

Matineja ndani miaka 30 kwa kuteka mtoto nyara na kumuua

May 27th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MAHAKAMA moja ya Afghan Stan Jumapili iliwafunga matineja wawili miaka 30 gerezaji, baada ya kuwapata na hatia ya kuteka nyara na kuua msichana, ambaye mauaji yake yalighadhabisha taifa hilo.

Mahsa Ahmadi ambaye alikuwa na miaka sita alitekwa nyara katika mtaa wa Kabul street mnamo Machi na akauawa baada ya wazazi wake kushindwa kulipa Sh30 milioni ili aachiliwe huru.

Baadaye polisi waliwakamata vijana wawili na wakatoa kanda ya video iliyowaonyesha wakikiri kuwa walitekeleza mauaji hayo.

Walisema kuwa walimteka nyara Mahsa na kumbeba kwa pikipiki hadi katika nyumba moja, kisha wakamnyonga walipokosa kupata pesa ambazo waliitisha.

Jaji aliwahukumu vijana hao, wote ambao wana umri chini ya miaka 18, miaka 30 jela, japo familia ya marehemu ikisema hukumu hiyo haikuwa adhabu tosha.

“Ninataka wapate adhabu kali zaidi, wanafaa kunyongwa. Wanafaa kuhisi jinsi tunahisi,” babake mtoto huyo akasema.

Lakini jaji huyo alisema kuwa kutokana na hali kuwa wawili hao si watu wazima, hawangepewa hukumu ya kunyongwa.