Michezo

Matokeo duni ya Shujaa, nusura iburute mkia tena #CapeTown7s

December 10th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA iliridhika na nafasi ya 13 kutoka orodha ya mataifa 16 yaliyoshiriki duru ya pili ya Raga ya Dunia iliyofikia kilele mjini Cape Town nchini Afrika Kusini Jumapili.

Shujaa, ambayo ilivuta mkia kwa kuambulia alama moja katika duru ya ufunguzi mjini Dubai mnamo Desemba 1 katika ligi hii ya mataifa 15 na duru 10, ilijiongezea alama tatu kutoka Cape Town kwa kuliza Wales 33-26 katika fainali ya kuamua nambari 13 na 14.

Vijana wa kocha Paul Murunga waliepuka kupigania nafasi mbili za mwisho baada ya kuchabanga mabingwa wa Afrika Zimbabwe 31-19 katika nusu-fainali ya kuorodheshwa kutoka nafasi ya 13 hadi 16.

Ushindi huu ulikuwa wa kwanza wa Kenya msimu huu baada ya kupoteza mechi tisa kutoka Novemba 30 msimu ulipoanza mjini Dubai. Ililemea Zimbabwe kupitia miguso ya Johnstone Olindi, Daniel Taabu, Dennis Ombachi na Vincent Onyala.

Taabu pia alichangia mikwaju miwili naye Olindi mkwaju mmoja. Olindi alikuwa mwiba dhidi ya Wales akichangia miguso mitatu nao Cyprian Kuto na Leonard Mugaisi wakafunga mguso mmoja kila mmoja. Taabu alifunga mikwaju minne dhidi ya Wales.

Kenya sasa ina jumla ya alama nne. Duru ijayo ya Raga ya Dunia itaandaliwa Hamilton Sevens nchini New Zealand mnamo Januari 26-27, 2019.