Michezo

Matokeo mseto kwa wanasoka wa Kenya wanaocheza ligi za kigeni

November 24th, 2020 5 min read

Na GEOFFREY ANENE

WANASOKA Wakenya wakiwemo Ismael Dunga, Joash Onyango na Joseph Okumu walikuwa katika orodha ya washindi kwenye ligi za kigeni wanazocheza mnamo Novemba 21 na Novemba 22.

Eric Johanna Omondi, Johanna Omolo, Clarke Oduor na Tera Luheni Alwyn pia walikuwa na siku nzuri ofisini, huku timu za nyota Victor Wanyama na Michael Olunga zikiumizwa. Haya hapa matokeo ya timu kutoka Bara Ulaya pamoja na Amerika na Canada, Tanzania, Afrika Kusini, Zambia na Japan zilizoajiri Wakenya.

ALBANIA

Mshambuliaji Ismael Dunga alifunga bao la ushindi Vllaznia ikibwaga mabingwa watetezi KF Tirana kwenye Ligi Kuu ya Albania hapo Jumamosi. Beki Herald Marku alipachika penalti iliyoweka Vllaznia bao 1-0 juu dakika ya 28 kabla ya Ernest Muci kusawazisha sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza. Marku alirejesha wenyeji Vllaznia kifua mbele 2-1 dakika ya 50, lakini mshambuliaji wa Ghana Derrick Sasraku akafanya mabao kuwa 2-2 dakika ya 63. Dunga aligonga msumari wa mwisho dakika ya saba ya majeruhi kupatia timu yake alama tatu muhimu zilizohakikisha Vllaznia inasalia kileleni mwa ligi hiyo ya timu 10. Imezoa alama tisa baada ya kushinda mechi zake tatu zote za kwanza.

BELARUS

Kiungo Mohammed Katana almaarufu Messi Agege alikuwa kitini timu yake ya Isloch Minskly Rayon ikipepetwa 2-0 na wenyeji Zhodino kwenye Ligi Kuu ya Belarus mnamo Jumapili. Isloch, ambayo imeambulia alama mbili pekee kutokana na mechi nne zilizopita, inapatikana katika nafasi ya saba kwa alama 44 baada ya kusakata mechi 29 kwenye ligi hiyo ya klabu 16.

UBELGIJI

Kiungo Johanna Omolo alitumiwa kama mchezaji wa akiba dakika 13 za mwisho timu yake ya Cercle Brugge ikizamisha Waasland-Beveren 2-0 kwenye Ligi Kuu nchini Ubelgiji. Muingereza Ike Ugbo alipachika mabao yote mawili baada ya kupokea mpira kutoka kwa Mholanzi Anthony Musaba dakika ya 43 na 82 mtawalia. Waasland-Beveren, ambayo bao lake lilikataliwa na teknolojia ya VAR dakika ya 33, ilikamilisha mechi wachezaji 10 baada ya beki kutoka Serbia Aleksandar Vukotic kuonyeshwa kadi nyekundu. Cercle inapatikana katika nafasi ya nane kwenye ligi hiyo ya klabu 18 ambayo ni ya mwisho ya kuingia Ligi ya Uropa. Imezoa alama 18 kutokana na michuano 12.

UINGEREZA

Barnsley anayochezea beki chipukizi Clarke Oduor ilizoa ushindi wake wa pili mfululizo na wanne katika mechi tano kwa kuchabanga Nottingham Forest 2-0 kwenye Ligi ya Daraja ya Pili ya Uingereza mnamo Jumamosi. Mabao ya kuchelewa kutoka kwa Callum Styles na Cauley Woodrow dakika chache baada ya Oduor kujaza nafasi ya Alex Mowatt dakika ya 82, yalitosha kunyanyua Barnsley nafasi sita hadi nambari 13 kwenye ligi hiyo ya timu 24. Barnsley imeambulia alama 16 kutokana na mechi 12 kwenye ligi hiyo inayoongozwa na Norwich.

GEORGIA

Kiungo Tera Luheni Alwyn alicheza mechi nzima timu yake ya Saburtalo Tbilisi ikibwaga Torpedo Kutaisi 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Georgia kupitia bao la mshambuliaji Giorgi Guliashvili hapo Jumamosi. Saburtalo ilikuwa imepoteza michuano mitano katika mashindano yote kabla ya kupata kitulizo dhidi ya Torpedo kwenye ligi hiyo ya timu 10. Inashikilia nafasi ya nne kwa alama 24 baada ya kutandaza mechi 16.

JAPAN

Mchana-nyavu matata Michael Olunga alipata bao lake la 24 kwenye Ligi Kuu ya Japan msimu huu, ingawa timu yake ya Kashiwa Reysol iliangukia pua baada ya kupigwa 2-1 na Sagan Tosu mbele ya mashabiki wake. Kashiwa ilikuwa ikisakata mechi yake ya kwanza tangu Oktoba 31 baada ya visa 16 vya maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa kambini mwake mapema Novemba na kulazimika kuingia karantini. Ilirejelea mazoezi Novemba 18, siku tatu kabla ya kualika Sagan uwanjani Kashiwa. Kashiwa ni ya 10 kwenye ligi hiyo ya klabu 18 kwa alama 41 kutokana na mechi 27.

AFRIKA KUSINI

Kiungo Anthony Agay Akumu alionjeshwa sekunde chache za mwisho timu yake ya Kazier Chiefs ikiokota alama moja katika sare ya 2-2 dhidi ya Golden Arrows kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini mnamo Jumamosi. Ilikuwa nipe-nikupe wakati Arrows iliona lango ya kwanza kupitia kwa Siboniso Conco dakika ya 49 nayo Chiefs ikasawazisha kupitia kwa raia wa Colombia Leonardo Castro dakika ya 58. Castro aliweka Chiefs mabao 2-1 juu dakika ya 65 kabla ya Nduduzo Sibiya kufanya mabao kuwa 2-2 dakika tano baadaye. Chiefs ni ya tisa kwa alama tano baada ya kusakata michuano minne. Mabingwa watetezi Mamelodi Sundowns anaochezea Brian Mandela Onyango waliadhibu AmaZulu 4-3 Jumapili. Beki Onyango, ambaye alijiunga na Mamelodi mwezi uliopita (Oktoba 29) kwa kandarasi ya miaka mitatu, yuko mkekani na jeraha. Mamelodi wamerukia uongozi kutoka nafasi ya tatu na kusukuma Swallows na Orlando Pirates katika nafasi ya pili na tatu, mtawalia. Mamelodi inaongoza ligi hiyo ya timu 16 kwa alama 10, mbili mbele ya Swallows na Pirates.

UHISPANIA

Beki Ismael Athuman Gonzalez hakuwa kikosi timu yake ya Las Palmas ikipoteza 3-1 dhidi ya wenyeji Sabadell kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Uhispania mnamo Jumapili. Sabadell ilivuna ushindi kupitia mabao ya Adrian Cuevas (mawili) na Gorka Guruzeta naye Sergio Ruiz akatinga goli la Las Palmas kujiliwaza. Beki wa Las Palmas Jonathan Silva Vieira kutoka Brazil alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 57.

USWIDI

AIK na Elfsborg wanazochezea mabeki Eric ‘Marcelo’ Ouma na Joseph Okumu ziliandikisha matokeo mseto nyumbani dhidi ya Orebro na Helsingborg kwenye Ligi Kuu ya Uswidi mnamo Jumapili. Timu ya AIK ilititigwa 2-0 kupitia mabao ya beki Eric Kahl (alijifunga) na mshambuliaji Mturuki Deniz Hummet. Elfsborg ililemea Helsingborg 2-1 kupitia mabao ya Per Frick (penalti) na Jeppe Okkels. Mwamerika Mix Diskerud alipachika bao la Helsingborg. Nayo Jonkopings Sodra anayochezea kiungo mshambuliaji Eric Johanna Omondi ilipepeta wenyeji Ljungskile 1-0 kwenye Ligi ya Daraja ya Pili Uswidi mnamo Jumamosi. Omondi alicheza dakika 81 katika mchuano huo ambao Jonkopings ikivuna alama tatu kupitia bao la mapema kutoka kwa Edin Hamidovic. Jonkopings inashikilia nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo ya timu 16 ambayo ni ya mwisho ya kupandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu msimu ujao. Nao viongozi Vasalunds watazuru nambari sita Sollentuna hapo Novemba 23. Vasalunds wameajiri beki Mkenya Anthony Wambani.

TANZANIA

Beki Joash ‘Berlin Wall’ Onyango alikuwa katika kikosi cha Simba SC kilichoaibisha wenyeji Coastal Union 7-0 mnamo Jumamosi. Katika mchuano huo ambao mabingwa watetezi Simba walikosa wachezaji muhimu Meddie Kagere, Luis Miquissone, Jonas Mkude na Chris Mugalu, John Bocco alifunga mabao matatu, Mzambia Cletus Chama (mawili) nao Hassan Dilunga na Mghana Bernard Morrison wakachangia bao moja kila mmoja. Kiungo Francis Kahata alikuwa kwenye benchi. Simba inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 23 kutokana na mechi 11 nayo Young Africans (Yanga) inayoajiri kipa Mkenya Farouk Shikalo iko alama moja mbele katika nafasi ya pili. Yanga ilitoka 1-1 dhidi ya Namungo uwanjani Benjamin Mkapa. Kipa Mkenya Farouk Shikalo hakuwa katika kikosi cha siku ya mechi. Biashara Mara United anayonoa kocha Mkenya Francis Baraza iko katika nafasi ya sita kwa alama 18 baada ya mechi yake ya 11 kutamatika 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji hapo Novemba 20.

AMERIKA & CANADA (MLS)

Kiungo Mkenya Victor Wanyama alikosa mechi ya awamu ya muondoano ya Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) timu yake ya Montreal Impact ikibanduliwa baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya New England Revolution, Jumamosi. Mhispania Carles Gil na raia wa Argentina Gustavo Bou walifunga mabao ya Revolution naye mshambuliaji wa Honduras Romell Quioto akapachika goli la Impact kufutia machozi. Wanyama hakuwa amejiunga na kikosi hicho nchini Amerika baada ya kuongoza Harambee Stars dhidi ya wanavisiwa wa Comoros kwenye mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) zilizosakatwa Novemba 11 na Novemba 15.

ZAMBIA

Kiungo Kelvin Kampamba alifungia Zesco United mabao yote miamba hao wakinyamazisha Kabwe Warriors 2-0 Jumamosi. Zesco ilianzisha Wakenya kipa Ian Otieno na mshambuliaji John Makwata. Makwata alipata bao katika kabla ya nusu saa, lakini likakataliwa akiwa amerombeza. Alikosa nafasi kadhaa nzuri kabla ya Zesco kupumzisha David Molinga na kuingiza mshambuliaji Mkenya Jesse Were dakika ya 51 ili kuongeza juhudi za kutafuta mabao. Kampamba aliweka Zesco kifua mbele dakika ya 66 kupitia frikiki safi kabla ya kuongeza la pili sekunde chache kipenga cha mwisho kilie. Naye kiungo Duncan Otieno alikuwa katika kikosi cha Lusaka Dynamos kilichotupa uongozi kikitoka 1-1 dhidi ya wageni Lumwana Radiants mnamo Jumamosi. Kiungo mshambuliaji Duke Abuya alianza mechi naye beki Harun Shakava alikuwa kwenye benchi timu yao ya Nkana ikikabwa 1-1 dhidi ya Zanaco uwanjani Nkana mnamo Jumapili.