Matokeo ya KCPE kutolewa mwezi huu

Matokeo ya KCPE kutolewa mwezi huu

VICTOR RABALLA na PIUS MAUNDU

MATOKEO ya mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) yanatarajiwa kutolewa baada ya wiki mbili.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha akiwa katika hafla ya usimamizi wa mtihani wa KCSE katika Kaunti Kisumu, alisema Jumanne kuwa usahihishaji wa mtihani wa KCPE unaendelea jinsi ilivyopangwa.

Alisema kuwa mtihani wa uandishi wa insha ya Kiswahili na Kiingereza unaendelea kusahihishwa na zinatarajiwa kumalizika hivi karibuni na matokeo kutolewa baada ya wiki mbili.

“Tumeanza kusahihisha insha na matokeo yanatarajiwa kutolewa baada ya wiki mbili. Ikiwa kutakuwepo na mabadiliko yoyote tutawajulisha,” alisema Prof Magoha.

Alisema kuwa idadi ya wanaosahihisha mtihani wa KCPE imepunguzwa kutokana na maagizo ya Wizara ya Afya kama njia ya kudhibiti kuenea kwa corona.

Kuhusu mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha nne (KCSE) unaoendelea, Prof Magoga alisema kuwa tayari wanafunzi 15 wamekamatwa na simu 15 kunyakuliwa.

Waziri huyo alisema kuwa wanafunzi wanaoshukiwa kuhusika katika udanganyifu katika mtihani wa kitaifa wataendelea kufanya mtihani wao uchunguzi ukiendelea.

“Tutawaacha wanafunzi wanaoshukiwa kuiba mtihani waendelee na mtihani wao mwaka huu 2021. Tutachunguza simu hizo na tukipata ushahidi katika simu hizo zinahusiana na uwizi wa mtihani, basi watachukuliwa hatua,” alisema Prof Magoha.

Alisema pia kuwa walimu wapatao 10 wamekamatwa kuhusiana na wizi wa mtihani.

Aliwaonya watahiniwa dhidi ya karatasi za mtihani zinazosambazwa kupitia mtandao wa kijamii akidai ni feki.

Kwingineko, upelelezi unaendelea kufanywa katika Kaunti ya Machakos, ambapo mwalimu mkuu wa shule ya Upili ya ABC Kiseveni ,Bi Betty Mutuku anadaiwa kuweka mtihani wa Hisabati kwenye mtandao wa Whatsapp kabla haujafanywa.

Afisa wa DCI katika kaunti ya Machakos, Bi Rhoda Kanyi alisema karatasi aliyoiweka mwalimu huyo katika Whatsapp ndiyo ilifanywa na watahaniwa wote nchini.

Mwalimu huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi Machakos huku polisi wakiendelea kukagua simu yake ili kudhibiti ukweli wa mambo.

“Tutakabidhi simu yake katika makao makuu ya DCI ili kung’amua jinsi alivyoipata karatasi hiyo ya mtihani,” Bi Kanyi alisema.

Bi Kanyi alisema kuwa ikiwa atapatikana na hatia, basi atachukuliwa hatua kali kulingana na Barasa la Kitaifa la Mtihani la Kenya.

You can share this post!

VITUKO: Bawabu amgeuzia mwalimu mkuu kibao cha wizi wa...

Bunge la kaunti lafungwa kuepusha ueneaji corona